Siri vipigo Yanga hii hapa

Muktasari:

Tangu ilipopata ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Welaytta Dicha ya Ethiopia, Yanga ilicheza mechi tisa mfululizo za mashindano mbalimbali bila kupata ushindi.

Dar es Salaam. Kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mwadui FC mkoani Shinyanga, Jumamosi iliyopita kimeifanya Yanga kuandika rekodi mbovu ya kucheza idadi kubwa ya mechi mfululizo bila kupata ushindi ambayo haijawahi kukutana nayo katika historia yake.

Tangu ilipopata ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Welaytta Dicha ya Ethiopia, Yanga ilicheza mechi tisa mfululizo za mashindano mbalimbali bila kupata ushindi.

Katika mechi hizo tisa ambazo Yanga ilicheza kwenye Kombe la Shirikisho na Ligi Kuu, imetoka sare mara tatu na kupoteza mechi sita huku ikifunga mabao mawili tu kwenye mechi hizo na nyavu zake zikitikiswa na mara 12.

Baada ya kuifunga Dicha hapa nyumbani, Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Singida United, ilifungwa 1-0 na Dicha ugenini, ilitoka sare 1-1 na Mbeya City, ilifungwa 1-0 na Simba, ilipoteza dhidi ya USM Alger kwa mabao 4-0 kabla ya kulala 2-0 ilipovaana na Prisons.

Mechi nyingine zilizofuata ni dhidi ya Mtibwa Sugar iliyofungwa bao 1-0, ilitoka suluhu na Rayon Sports kabla ya kunyukwa 1-0 ilipomenyana na Mwadui.

Kigogo avunja ukimya

Mjumbe wa Kamati ya Mashindano Yanga, Athumani Kihamia amefichua kwamba udhaifu wa kiutendaji ndani ya klabu hiyo umechangia kuidhoofisha Yanga.

Kigogo huyo alisema wachezaji na makocha wanafanya kazi kubwa na hawastahili kubeba lawama ambazo mashabiki wamekuwa wakizitoa kutokana na timu kufanya vibaya.

Kihamia alisema kuna mpasuko mkubwa ndani ya Kamati ya Utendaji aliodai kuwa umechangia timu hiyo kutopata maandalizi mazuri kabla ya mechi na kujikuta ikipoteza.

“Ni vigumu wachezaji kufanya vizuri uwanjani kama madai ya mishahara na posho hayajalipwa. Nilitarajia kipindi kama hiki, Kamati ya Utendaji ichukue hatua stahiki kuhakikisha timu inakuwa kwenye hali nzuri.

“Lakini kwa bahati mbaya, tangu Mwenyekiti Yusuf Manji alipojiuzulu, Kamati ya Utendaji ni kama haipo na badala yake kazi nzito imekuwa ikifanywa na Kamati ya Mashindano katika kusaka fedha na kuwatunza wachezaji jukumu ambalo lilipaswa kusimamiwa na kamati hiyo,” alisema Kihamia.

Kihamia alisema ipo haja kwa Kamati ya Utendaji ya Yanga kutafuta suluhisho la matatizo yanayoikabili timu hiyo vinginevyo hali itazidi kuwa mbaya.

“Tumeshakosa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA jambo lililotufanya tukose nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa. Hili sio jambo zuri kwa klabu kubwa na yenye heshima kama Yanga.

Kigogo huyo alisema Kamati ya Utendaji inapaswa kukutana kusuka mikakati ya kuhakikisha Yanga inashiriki kikamilifu mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha afunguka

Kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila alisema ratiba ya kucheza mechi nyingi mfululizo, kuwakosa wachezaji muhimu na kitendo cha kutokuwepo benchi kwa kocha mkuu, Mwinyi Zahera ni miongoni mwa sababu zinazoigharimu Yanga.

“Tunawakosa wachezaji muhimu kutokana na majeraha, pia kama unavyoona ratiba ya ligi inatulazimisha tucheze mechi nyingi ndani ya muda mfupi jambo linalofanya wachezaji kuchoka.

Kingine kama unavyoona kocha mkuu hakuwa anakaa kwenye benchi wakati mechi zinachezwa, hivyo kuna wakati inatupa wakati mgumu hasa katika kufanya maamuzi ya kiufundi,’ alisema Mwandila.

Kauli ya Mkwasa

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alisema uongozi ulifanya kazi kwa nafasi yake na walikuwa na mipango mizuri katika maandalizi ya timu, lakini wachezaji majeruhi walikuwa kikwazo kutimiza ndoto yao.

“Uongozi umeona changamoto zote tunachoweza kusema tutazifanyia kazi na msimu ujao tutarejesha kombe mikononi mwetu, tunafarijika majeruhi waliokuwa kwenye timu wamepona na kurejea, msimu ujao mambo yatakuwa mazuri,” alisema Mkwasa.

Yanga leo inateremka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kupepetana na Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.