SportsPesa yazipiga mkwara Simba, Yanga

Muktasari:

  • Klabu kongwe za Simba na Yanga zimeonywa kuacha kutumia wachezaji vijana katika mashindano ya SportPesa, yanayotarajiwa kufanyika Januari 22 hadi 27, mwaka huu.

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa Kampuni ya SportPesa,Tarimba Abbas, amezionya Simba na Yanga kuacha kuleta timu za vijana katika mashindano ya msimu ujao.

Mashindano ya SportPesa yanatarajiwa kuanza Januari 22 hadi 27, mwakani kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.

Tarimba alisema Simba na Yanga zimekuwa na desturi ya kuleta timu dhaifu katika mashindano hayo hatua inayosababisha kushindwa kutwaa ubingwa.

"Mwaka huu hatutaki mzaha katika mashindano haya miaka miwili Gor Mahia imechukua ubingwa  na kucheza na Everton hapa hapa Tanzania na England.

"Hatutaki hicho kitu kitokee tena, kukosa ubingwa kwa timu za Tanzania kunatokana na klabu kuleta vikosi vya majaribio. Sasa mwaka huu hatutaki mfanye hivyo tunahitaji timu moja ya Tanzania iwe bingwa.

Tarimba alisema mashindano ya SportsPesa yatafanyika katikati ya Ligi Kuu, hivyo ni fursa kwao kupeleka timu zinazoundwa na wachezaji wanaocheza katika mashindano hayo.

Mashindano ya msimu huu yatashirikisha timu nane za Yanga, Simba, Singida United na Mbao Tanzania, Gor Mahia, Bandari, AFC Leopards na Kariobangi Sharks za Kenya.

Pia Tarimba  alisema wameiteua Mbao kuwa timu mwalikwa katika mashindano hayo kwa kuwa imekuwa ikitoa ushindani uwanjani katika mechi za Ligi Kuu.