Stand United wanajipanga balaa

Muktasari:

  • Timu hiyo kwa sasa inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

 Katibu wa Stand United 'Chama la Wana, Kenny Nyangi amesema watawaongeza  wachezaji sita  wazoefu na tayari walishamalizana na Juma Abdallah kutoka Mbeya City.

Nyangi alisema wengine wanatarajia kumalizana nao jioni ya leo, wawili wakitokea Zanzibar na amesisitiza kwamba hawajakurupuka kuwasajili kwani waliwafanyia majaribio katika mazoezi.

"Wachezaji ambao tutawaongeza tulikuwa tunafanya nao mazoezi, tunahitaji kuwa na mabadiliko kutokana na mwanzo wetu hakuwa mzuri, lazima tujipange vilivyo ili tusije tukashuka daraja," alisema Nyangi.

Nyangi anakiri namna walivyochemka usajili wa mwanzo wa msimu kwa kusajili wachezaji kutoka vijijini, waliokuwa wanajishugulisha na kazi ya ukulima na mwisho wa siku wakashindwa kufikia malengo.

"Hatukuwa na amani kila tulipokuwa tunacheza mechi, lakini kwa sasa lazima tufanye kitu makini,kitakachofanya tuvuke katika nafasi mbaya, kutokana na mzunguko wa pili kuwa mgumu zaidi," alisema.

Amezungumzia udhamini walioupata kwamba utawapa tafu ya kuhakikisha wanafanikisha mambo yao kwa wakati, ikiwemo malipo ya wachezaji wao.

"Hakuna kitu kizuri kama wachezaji kuwapa haki zao kwa wakati, wanakuwa na moyo wa kujituma kwa bidii wakijua watafutwa jasho,"alisema Katibu huyo.