Stand United yapandisha makinda wao na kusajili watano

Muktasari:

  • Stand United waliingia hatua ya fainali ya michuano ya kombe la vijana chini ya miaka 20 na wakafungwa na Mtibwa Sugar bao 1-0.

Mwanza. Wameula mwanangu kwani Kocha Msaidizi wa Stand United, Athumani Bilali 'Bilo' amesema, wamewapandisha wachezaji wao kutoka kwenye kikosi  cha timu ya vijana na sasa watajiunga na ile ya wakubwa.

Wachezaji hao wamepandishwa kwenye timu ya wakubwa baada ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Uhai iliyomalizika wiki iliyopita jijini Dodoma na ubingwa ukichukuliwa na Mtibwa Sugar huku Stand United wakinyakua nafasi ya pili.

Vijana hao waliopandishwa ni pamoja na Morris Maela, Majid Kimbondile, Makenzi Kapinga,  John Rwitiko, Frank Zakaria na Abel Yegela.

Amesema kutokana na kiwango walichokionyesha kwenye Uhai Cup hawana wasiwasi kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara msimu ujao.

“Hawa wachezaji walifanya vizuri kwenye mashindano ya Uhai Cup, nikaona wanaweza kutusaidia pia kwenye ligi kuu katika pindi cha msimu ujao hivyo nimependekeza wapandishwe, "alisema Bilo.

Hata hivyo, Bilo aliongeza kuwa baada ya hapo watasajili wachezaji watano wakiwemo wale wa kigeni ma lengo ni kuwa na timu bora itakayofanya vizuri  ligi kuu.

“Tunataka msimu ujao tuwe na timu bora itakayofanya vizuri kwenye ligi pamoja na Kombe la FA hivyo usajili wetu utakuwa makini zaidi ya ule uliopita ambao tulianza vibaya baada ya kushindwa kuchagua wachezaji wenye viwango,” alisema Kocha huyo.