Stand Utd, Mtibwa Sugar hapatoshi fainali Uhai Cup

Muktasari:

  • Stand United imetinga fainali hiyo baada ya juzi kuwatandika Azam FC bao 1-0 katika mtanange wa Nusu fainali uliopigwa katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dodoma jijini Dodoma.

Mwanza.Wakati Stand United ikitarajia kuwavaa Mtibwa Sugar kesho Alhamisi katika mpambano wa fainali ya Uhai Cup, Kocha wa timu hiyo Athumani Bilali “Bilo”amewataka mashabiki wa soka mkoa Shinyanga kuandaa pilau la kutosha kwani lazima warudi na ubingwa.

Stand United imetinga fainali hiyo baada ya juzi kuwatandika Azam FC bao 1-0 katika mtanange wa Nusu fainali uliopigwa katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dodoma jijini Dodoma.

Kwa upande wao Mtibwa Sugar walitinga fainali hizo baada ya kuwafunga mabingwa watetezi  wa Mashindano hayo Simba SC kwa bao 1-0.

Kocha Bilo alisema kikosi chake kipo sawa kuelekea mchezo huo wa fainali ambapo amesema Mtibwa Sugar wanafungika kirahisi hivyo mashabiki wa Shinyanga wajiandae kupokea ubingwa huo.

Alisema Shinyanga wanatakiwa kuanza kuandaa pilau la kusherekea ubingwa huo kwani vijana wake wana morali kubwa ya kuwafunga Mtibwa Sugar kwenye fainali hiyo.

“Iko hivi tumejipanga kurudi na hili Kombe nyumbani Shinyanga hawa Mtibwa Sugar wanafungika tu hivyo mashabiki wasiwe na wasiwasi kwenye fainali hii”alisema Bilo.

Kwa upande wake Straika Moris Maela  wa Stand United alisema wao kama wachezaji wamejipanga vilivyo kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mpambano huo.

“Najua mchezo utakuwa mgumu lakini sisi tumejipanga kikamilifu kuweza kupata ushindi kwani lengo letu ni kutwaa huu ubingwa”alisema Maela.