Stars leo kufa au kupona

Muktasari:

  • Taifa Stars leo inashuka dimbani kuikabili Lesotho
  • Dua za Watanzania wote leo zinaelekezwa Lesotho ambako Stars inacheza bila ya nahodha wake Samatta, Kapombe na Mandawa.

Dar es Salaam/Maseru. Tanzania leo italazimika kucheza kwa nguvu zote kupata pointi tatu nyeti zitakazoamua hatma yake katika michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) itakaporudiana na wenyeji Lesotho kwenye Uwanja wa Setsoto mjini Maseru.

Lesotho, inayokamata mkia katika Kundi L baada ya kuambulia pointi mbili tu, nayo imepania kucheza kwa kushambulia kuanzia dakika ya kwanza ili angalau ishinde na kufufua matumaini ya kufuzu kwenda Cameroon kwenye fainali hizo mwakani.

Uganda imeshafuzu kutoka Kundi L ikiwa na pointi 13 baada ya jana kuilaza Cape Verde kwa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa mjini Kampala.

Tanzania inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tano, na ushindi dhidi ya Lesotho utaimarisha nafasi yake katika Kundi L na hivyo kuwa na matumaini ya kuungana na Uganda kwenda Cameroon.

Cape Verde, ambayo ililazwa mabao 2-0 na Tanzania jijini Dar es Salaam ikiwa kulipizwa kisasi baada ya kushinda kwa mabao 3-0 nyumbani mjini Praia, baada ya kipigo cha jana imebaki na pointi nne.

Tanzania iliweka kambi ya takriban siku kumi jijini Johannesburg chini ya kocha Emmanuel Amunike na juzi ilihamia Maseru tayari kwa mchezo huo muhimu.

Amunike, nyota wa zamani wa Barcelona na mfungaji wa bao lililoipa Nigeria medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki mwaka 1996, anatatarajia upinzani mkali kutoka kwa wenyeji waliolazimisha sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo jijini Dar es Salaam, wageni wakisawazisha kwa mpira wa adhabu mwishoni mwa mchezo.

Hata hivyo, moto ulioonyeshwa na vijana wake katika mechi ya marudiano na Cape Verde, utampa faraja ya Taifa Stars kufanya vizuri zaidi dhidi ya wenyeji wao ambao wanashika nafasi ya 149 kwa ubora duniani.

Nahodha Mbwana Samatta, ambaye alipika bao la kwanza na kufunga la pili dhidi ya Cape Verde, leo hatakuwepo uwanjani kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano alizopata katika mechi zilizopita, matarajio yote ya Tanzania leo ni kwa Simon Msuva na Shiza Kichuya, ambaye huenda akapangwa nafasi ya Gadiel Michael, ambaye anaonekana kutoimudu nafasi ya winga wa kushoto.

Kichuya na Msuva watakuwa mbele ya viungo watatu -mkongwe Erasto Nyoni, Mudathir Yahya na Himid Mao- kama ilivyokuwa katika mchezo na Cape Verde baada ya Mao kupwaya katika mechi ya kwanza na kumlazimisha Amunike kumuongeza Shomari Kapombe kuituliza timu ingawa naye leo hayupo.

Kipa Aishi Manula anatarajiwa kulindwa na Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Hassan Kessy na Abdul Banda, ukuta ambao uliidhiihiti safu ya ushambuliaji ya Cape Vedre katika mchezo uliopita jijini Dar es Salaam na Stars kuibuka na ushindi uliofufua matumaini ya kufuzu.

Lakini kocha wa Lesotho, Moses Maliehe alisema ili nchi yake iweze kufuzu ni lazima waishinde Tanzania leo, baada ya kulazimisha sare kwenye Uwanja wa Azam kwa bao lililofungwa na Thapelo Tale.

Maliehe amesema wacheaji wa timu yake, maarufu kwa jina la Likuena au Mamba, watalazimika kuipigania nchi na wamepanga kuishambulia Stars kuanzia mwanzo.

“Tuko tayari, mazingira yanafanana (kama ilivyokuwa) mechi ya Uganda, na tumepanga kushambulia kuanzia mwanzo wa mchezo,” Maliehe aliiambia tovuti ya gazeti la The Post.

“Tumejiandaa vya kutosha kucheza na Tanzania; lazima tushinde mchezo na hatuwezi kuzungumzia kushinda mechi bila ya kushambulia. Hatuna mpango mwingine wowote zaidi ya kushambulia.”

Likuena itamkosa mshambuliaji wake Nkoto Masoabi anayechezea Real King ya Afrika Kusini na ambaye wiki mbili zilizopita aliifungia timu hiyo bao ilipotoka sare ya mabao 2-2 na Ajax Cape Town.

Lakini Maliehe alidokeza kuwa mshambuliaji wa timu ya Magereza ‘Lesotho Correctional Services’, Thapelo Tale atakuwa jibu.

“Ni bahati mbaya hatutakuwa naye, lakini tunaye Thapelo Tale, ni mchezaji mwenye kasi,” alisema.

Kocha huyo alisema ameteua kikosi bora kwa ajili ya mechi hiyo na kwamba wana taarifa za kutosha kuhusu kikosi cha Tanzania zitakazowawezesha kupata ushindi leo na kufufua matumaini.