Straika Kiyombo awapigia hesabu Okwi, Chirwa

Muktasari:

Kiyombo yupo nafasi ya pili akiwa na mabao saba sawa na nyota wa Prisons, Mohamed Rashid wakitanguliwa na Emanuel Okwi (Simba) mwenye mabao nane, huku Chirwa akiwa na mabao sita.

Mwanza. Achana na Tuzo ya Mchezaji Bora aliyoipata ya mwezi Desemba yule nyota wa Mbao FC, Habib Kiyombo, kwani kinda huyo amesema kuwa kiu yake ni kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu.

Straika huyo hadi sasa ameweka rekodi kwenye Kombe la FA baada ya kufunga mabao matano katika mchezo mmoja ambapo waliwabamiza Makanyagio FC ya Katavi mabao 5-0.

Kiyombo alisema kuwa tuzo aliyoipata ya mchezaji bora kwa mwezi uliopita anaiona kama moja ya njia ya kufikia malengo yake ya kutwaa kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora.

“Kwanza namshukuru Mungu,ile tuzo naona kama ni moja ya njia yangu kuelekea kule napopatamani,kiu na ndoto yangu ni kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu tu”alisema Kinda huyo.

Alisema kuwa kwa tuzo hiyo pia ni changamoto kwake kuhakikisha anajituma zaidi ili kuweza kuwapoteza washindani wake,Okwi na wengineo ambao wanaonyesha ushindani.

Alisisitiza kuwa atapambana kila mchezo kwake kutupia japo bao moja ili kuzidi kujiweka mazingira mazuri,huku akihakikisha anaisaidia Mbao kuwa nafasi nzuri kimsimamo.

“Ushindani ni mkubwa,lakini nitapambana kadri niwezavyo kuweza kutupia japo bao moja kila mchezo ili niwapoteze kabisa wapinzani wangu kama yule Okwi na Rashid”alitamba Kiyombo.