TFF wakata rufaa kupinga Wambura kurejeshwa

Muktasari:

  • Michael Wambura, ambaye ni makamu wa rais wa TFF, alifungua kesi Mahakama Kuu kutaka ifanye marejeo ya uamuzi wa Kamati ya Rufaa ya Maadili ya shirikisho hilo na ikabaini kuwa katiba haikufuatwa katika kumfungia maisha kujihusisha na soka.

Dar es Salaam. Nia ya Michael Wambura kurejea katika wadhifa wake wa makamu wa rais wa Shirikisho la Soka (TFF), itabidi isubiri muda zaidi baada ya chombo hicho kuamua kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutengua adhabu yake ya kufungiwa maisha.

Wambura, ambaye bamekuwa na migogoro na mamlaka za soka kwa miaka kadhaa sasa, alifanikiwa kuishawishi Mahakama Kuu kukubaliana na hoja zake kuwa Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufaa ya Maadili za TFF hazikuzingatia katiba ya shirikisho hilo wakati zilipofikia uamuzi wa kumfungia maisha kujihusisha na soka.

Wambura aliiomba Mahakama Kuu irejee uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Rufaa ambayo ilikubaliana naye, kitu kilichomaanisha kuwa anarejea katika wadhifa wake wa makamu wa rais na mjumbe wa kamati ya utendaji.

Lakini jana, katibu mkuu wa TFF, Wilfred Kidao aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamekata rufaa dhidi ya uamuzi huo ambao unamrejesha Wambura katika nafasi yake, hali ambayo itamfanya katibu huyo wa zamani wa Chama cha Soka (FAT) kusubiri hadi shauri hilo litakapomalizika.

Kidao alisema wameamua kufikia hatua hiyo baada ya kukaa chini na mwanasheria wao, Alex Mgongolwa.

"Mwanasheria wetu ametushauri kwamba tukate rufaa dhidi ya Michael Wambura na tayari tumeshafanya hivyo. Tunasimamia katiba yetu ya TFF na ndio inayotuongoza," alisema Kidao.

Pia Kidao alizungumzia mjadala ulioibuka wakati Wambura aliposema anakwenda TFF kurejea kazini baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi huo, kutokana na baadhi kusema hana ofisi katika majengo ya shirikisho hilo na wengine kusema anastahili kuingia ofisini baada ya uamuzi wa mahakama.

"Mimi ndio mwenye ofisi kwa sababu ni mtendaji mkuu, lakini hata Rais Karia mwenyewe ana ofisi ya ambayo inatumika kwa mikutano na sio mtu wa kukaa sana ofisini kwa sababu ni muajiriwa wa Serikali," alisema.

Wambura, ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Mara, amekuwa na migogoro na mamlaka za uendeshaji soka kwa muda mrefu.

Wakati akiwa katibu mkuu wa FAT, aliingia kwenye mgogoro na mwenyekiti wake wa wakati huo, Muhidin Ndolanga uliosababisha Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) liingilie kati na kupendekeza chama hicho kiwe na katibu mkuu wa kuajiriwa.

Hata mapendekezo hayo ya Fifa hayakupokelewa vizuri; Ndolanga aliyakubali lakini Wambura akayapinga. Hata hivyo, wawili hao walifikia muafaka na kukubaliana kupinga mapendekezo ya Fifa.

Akiwa kiongozi Simba, Wambura aliingia kwenye mgogoro na viongozi wenzake, hali iliyosababisha aende mahakamani na hivyo kujikuta akijitia doa ambalo mara kadhaa limemzuia kugombea nafasi katika uongozi wa soka hadi rais aliyepita, Jamal Malinzi alipotangaza msamaha kwa wote waliofungiwa baada ya kushinda uchaguzi mwaka 2013.