TFF yakiri udhaifu Ligi Kuu

Muktasari:

  • Wambura alisema suala la viwanja ni changamoto kubwa  na hivyo kupelekea ratiba wakati mwingine kuvurugika.
  • Alisema viwanja mbalimbali vinavyotumika kwa ligi pia vimekuwa vikitumika kwa kazi nyingine zikiwemo za kijamii hivyo kuvifanya viwanja hivyo kutokuwa katika hali nzuri .

Dar es Salaam. Mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura amefurahishwa na jinsi Ligi Kuu Bara inavyoenda vizuri lakini amekiri kuwa kuna changamoto kubwa ya viwanja.

Wambura alisema suala la viwanja ni changamoto kubwa  na hivyo kupelekea ratiba wakati mwingine kuvurugika.

Alisema viwanja mbalimbali vinavyotumika kwa ligi pia vimekuwa vikitumika kwa kazi nyingine zikiwemo za kijamii hivyo kuvifanya viwanja hivyo kutokuwa katika hali nzuri .

"Hii ni changamoto kubwa tunayokutana nayo kwenye ligi kwani unaweza mkavifanyia ukaguzi viwanja tayari kwa ligi lakini  baada ya siku tatu unakuta  viko tofauti na hiyo yote inasababishwa na  viwanja hivyo vinatumika kwa kazi nyingine zaidi ya mpira.

"Ukiangalia hata mechi ya Simba na Mbao ambayo tulitamani ichezwe mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa CCM Kirumba ilibidi katika ratiba tuipange Alhamis kwa sababu Jumamosi na Jumapili kuna shughuli ya kijamii kwenye uwanja huo"alisema Wambura.

Simba inaondoka leo kwa ndege kwenda Mwanza tayari kwa mchezo huo. Msimu uliopita kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza Simba ilibidi ifanye kazi ya ziada baada ya kutoka nyumba kwa mabao 2-0 na kushinda kwa mabao 3-2.

Hata hivyo habari zinadai kuwa Uwanja huo wa CCM Kirumba Mwanza , Jumamosi utatumika kwa ajili ya tamasha la burudani la Fiesta linaloandaliwa na Clouds Media na ndio maana mechi hiyo ya Mbao na Simba ikarudishwa Alhamisi.