TFF yabadili viwanja Kombe la FA

Muktasari:

Bingwa wa Kombe la FA anapata tiketi ya moja kwa moja kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limezibeba Yanga, Azam na Mtibwa Sugar kwa kubadilisha viwanja vitakavyotumika kwa mechi za raundi wa 32 ya Kombe la Shirikisho (ASFC).

Mkurugenzi wa mashindano wa TFF, Efrem August alisema wameamua kufanya mabadiliko ya viwanja kutokana na sababu mbalimbali.

"Kulikuwa na sintofahamu kwenye michezo mitatu kuhusu viwanja, michezo hiyo ni Majimaji Rangers dhidi ya Mtibwa Sugar, Shupavu dhidi ya Azam na ule wa Ehefu na Yanga.

"Michezo hiyo imehamishiwa kwenye viwanja vingine, vile vya mwanzo havikukidhi vigezo, Majimaji Rangers itacheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Ilulu, wakati Shupavu itaivaa Azam kwenye Uwanja  wa Jamhuri wa Morogoro, wakati Ehefu itawakaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya," alisema August.