Tanzania yavuna medali saba Japan

Muktasari:

Wanariadha wa Tanzania wamepata medali saba zikiwemo nne za dhahabu katika mashindano ya mbio za Nagai Marathoni zilizofanyika mwishoni mwa wiki nchini Japan.

Dar es Salaam.Wanariadha wa Tanzania wameweka rekodi kwenye mbio za Nagai Marathoni, baada ya kutwaa medali saba zikiwemo nne za dhahabu.

Katika mbio hizo zilizofanyika jana nchini Japan, Tanzania ilitwaa ubingwa kwenye marathoni (kilomita 42) kwa wanaume na wanawake na medali kama hizo kwenye nusu marathoni.

Wanariadha walioshinda dhahabu ni Marco Joseph aliyekimbia saa 2:21:13 na Angelina John aliyetumia saa 2:43:21 kumaliza mbio.

Dhahabu nyingine ilichukuliwa na Fabiano Sulle kwenye nusu marathoni aliyekimbia kwa saa 1:02:53 na Amina Mohammed aliyekimbia kwa saa 1:16:08 akichukua upande wa wanawake.

Kwenye mbio hizo za nusu marathoni kwa wanawake, Tanzania iling'ara baada ya kuchukua medali ya kwanza hadi ya tatu.

 Rozalia Fabian aliyekimbia kwa saa 1:18:57 alitwaa fedha na Sylivia Masatu aliyekimbia kwa saa 1:32:52 alihitimisha tatu bora.

Kwenye marathoni wanaume,Wilbard Peter aliyekimbia kwa saa 2:32:12 alitwaa medali ya fedha.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelim Gidabuday alisema matokeo hayo ni faraja kwa Tanzania na yanatoa taswira nzuri kwenye mchezo huo.

Wakati huo huo, wanamichezo walioshiriki Olimpiki ya vijana wametaja hali ya hewa Argentina imewakwamisha kutwaa medali.

"Baridi ilikuwa kali mno Argentina, kuna wakati tuliona kama miguu inaganda, ilituchukua muda kidogo kuzoea hali ya hewa," alisema  nahodha Regina Mpigachai ambaye ni mwanariadha.

Regina alimaliza wa kwanza katika kundi lake katika mbio za mita 800 za raundi ya pili na raundi ya kwanza alishika nafasi ya saba.

Francis Damiano alimaliza wa nne mbio za kilomita nne alimaliza nafasi ya nne na 12 mita 3,000. Waogeleaji, Denis Mhini na Sonia Tumiotto walishindwa raundi za awali. Timu hiyo iliwasili nchini jana.