Tanzanite Queens yatuma salamu Ligi Kuu

Muktasari:

Timu ya Tanzanite Queens imepania kufanya kweli katika mashindano ya Ligi Kuu Wanawake baada ya kupanda daraja.

Kocha wa timu hiyo Abdallah Juma alisema ana matumaini ya kufanya vyema katika mashindano hayo baada ya kusajili wachezaji sita wapya.

Arusha.Tanzanite Queens ya Arusha, imeahidi kufanya mapinduzi katika soka, itakaposhiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kocha wa Tanzanite Queens, Abdallah Juma, alisema maandalizi waliyofanya yatawawezesha kushindana na kutwaa ubingwa wa ligi hiyo itakayoanza Novemba 24.

Alisema kufanya vyema katika ligi hiyo kutaongeza ushawishi kwa wakazi wa Arusha kuwaunga mkono kwenye mashindano hayo ya soka kwa wanawake.

Timu hiyo inayomilikiwa na Kampuni ya Tanzanite 2014, ilipanda daraja baada ya kufanya vizuri kwenye ligi ndogo mwaka huu ikiwa  timu pekee ya Mkoa wa Arusha kushiriki Ligi Kuu.

Juma alisema wanataka kuwaonyesha wadau soka walistahili kucheza Ligi Kuu kwa kulitwaa ubingwa wa Serengeti (SPL).

“Tumefanya maandalizi ya kutosha tuliweka kambi ya muda mrefu tangu mwezi uliopita, tumeongeza wachezaji sita wapya kutoka Simba Queens, Ever Green za Dar es Salaam na Panama ya Iringa,”alisema Juma.

Baadhi ya timu zitakazoshiriki ni Yanga Princes, Simba Queens, Ever Green, JKT Queens (Dar es Salaam), Mlandizi Sisters (Pwani), Allans Queens, Baobao (Dodoma), Panama (Iringa), Sisterz FC (Kigoma) na Marsh Academy ya Mwanza.