Tegete: Kupaki basi kutawagharimu Mbao

Muktasari:

Mbao FC iliweka rekodi ya kucheza fainali ya Kombe la FA katika msimu wake wa kwanza mwaka jana

Mwanza. Kocha wa zamani wa Toto Africans, John Tegete amewaambia Mbao FC mtindo wao wa kucheza kwa kulinda sana kuliko kushambulia utawagharimu kwenye Ligi Kuu mzunguko huu.

Mbao FC ina pointi 19 ikiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu wameshinda mechi nne, sare saba na kufungwa saba.

Tegete alisema Mbao FC imekuwa ikicheza kwa kujilinda kuliko kushambulia jambo ambalo linawanyima ushindi katika michezo mingi.

Alisema mfumo wa kulinda unatokana na aina ya mechi husika, lakini si kila mchezo wa ligi ufanye hivyo, hata mechi za nyumbani Mbao FC wanatumia muda mwingi kuzuia kuliko kushambulia.

“Unajua kulinda sana kunategemea kama uko ugenini lakini wao hata mechi za nyumbani wanacheza soka la kujilinda sana hii kitu kamwe uwezi kupata ushindi kwa kuwa utakuwa ufungi mabao,” alisema Tegete.

Tegete alisema Ligi Kuu msimu huu imekuwa ngumu hivyo kama Mbao FC wakiendelea na hali hiyo basi watajikuta wamerudi Daraja la Kwanza msimu ujao.