Tiketi za elektroniki zazua balaa

Muktasari:

  • TFF iko katika mchakato wa kutumia tiketi za elektroniki ili kuokoa mapato ya milangoni.

Mbeya. Utoaji tiketi za ki-eletroniki kwenye mechi ya kirafiki iliyozikutanisha timu za Mbeya City na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, umeingia dosari baada ya wengi kutoingia uwanjani kwa madai ya kukosa tiketi.

Uchunguzi wa waandishi ulijionea vijana wengi wakihaha nje ya uwanja kusaka tiketi wakati timu zikiendelea kucheza na idadi ndogo ya mashabiki wakishuhudia.

Vijana hao walilalamikia maandalizi wakisema wamekosa tiketi kutokana na mfumo mpya wa kielektroniki.

Mchezo huo uliandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) maalumu kwa ajili ya kuufanyia majaribio utaratibu wa kuuza tiketi za kielektroniki, ambazo zitaanza kutumika kwenye viwanja mbalimbali nchini msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Akizungumzia malalamiko ya mashabiki waliokosa tiketi, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema waliokosa ni wale waliokuwa na mazoea ya kununua tiketi kwenye milango ya uwanja.

“Kwa mfumo huu mpya tiketi haziuzwi uwanjani bali kwenye vituo maalumu vinavyotangazwa,” alisema na kusisitiza kwamba ni lazima wapenzi wa soka wafuate utaratibu huo.

Wambura alisema baada ya kuona mashabiki wengi wamefika uwanjani wakiwa na fedha mkononi walilazimika kumtafuta wakala mmoja aliyekuwa ameandaliwa kuuza tiketi hizo kwenda kuzichukua dukani kwake na kufika nazo uwanjani kwa ajili ya kuwauzia.

Kutokana na hali hiyo, ghafla walizuka wajanja ambao walizinunua tiketi nyingi kutoka kwa wakala huyo na kuanza kuziuza kwa Sh5,000, jambo ambalo lilisababisha kero.

Wambura alisema hiyo ni changamoto nyingine huku akibainisha pia kwamba na ulinzi ulikuwa dhaifu milangoni.