Dodoma FC yatamba kutinga Ligi Kuu

Muktasari:

  •  Dodoma FC iko katika nafasi ya pili na pointi 18 mara baada ya kuipisha timu ya Alliance School ya Mwanza yenye pointi 19 ikifuatiwa Biashara yenye pointi 17 na pamba yenye pointi 12.

Timu ya Dodoma FC ya mkoani hapa, wamejinasibu kuwa hakuna kitu kitakachoweza kuwazuia kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Dodoma FC imefikia hatua ya kusema hivyo kama kujibu malalamiko ya wadau wa soka mkoani hapa walioingiwa na mashaka kuhusu kupanda VPL msimu ujao kwa timu yao kufuatia kufanya vibaya katika mechi zake mbili za mwisho kabla ya mapumziko ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili.

Dodoma FC ilijikita kileleni mwa kundi C' kwa kipindi chote cha mechi za Ligi Daraja la Kwanza, kufuatia matokeo mazuri waliyokuwa wanayopata, lakini mzunguko wa pili umewaanzia vibaya mara baada ya kufungwa mechi mbili mfululizo ikiwemo ya hivi karibuni dhidi ya pamba huko Mwanza. 

Katibu mkuu wa Dodoma FC Fourtnatus Johnson alisema kuwa nafasi yao ni namba moja hivyo mapema mechi ya Desemba 16 mara baada ya dirisha dogo la usajili kufungwa lazima warudi katika nafasi yao kwa kuvuna pointi tatu. 

"ligi daraja la kwanza ni ngumu asikuambie mtu, lakini Tunashukuru Mungu hatuko katika nafasi mbaya, hivyo niwaambie wadau wetu wa Dodoma wasiwe na wasiwasi kwani mwakani lazima tucheze ligi kuu hivyo matokeo yasiwatishe"

Alisema kuwa kwa sasa wanasubiri ripoti ya kocha wao Jamhuri Kiwelu "Julio" juu ya wachezaji watakaofanikiwa kubaki na wanaondoka ili kujua nafasi za kufanya usajili ili kukazia kikosi chao katika makali ya kuhakikisha wanatimiza ndoto za wana Dodoma kushuhudia Ligi Kuu

"Niwaombe Shirikisho la Soka nchini waache timu zicheze mpira na matokeo yaamue siyo kuangalia kanda wanazotoka iwe kigezo cha kupigania timu husika zipate hata kama kiwango chao cha kucheza ni mbovu."