Ubingwa Bara Simba, Yanga hesabu kali

Muktasari:

Timu hizo zimeweka kambi mkoani Morogoro kujiandaa na mchezo huo, lakini Simba inarejea Dar es Salaam leo.

Kama ulikuwa unaamini mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga, Jumapili hii utaamua bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, basi ujue umekosea.

Tathmini iliyofanywa na gazeti hili imebaini matokeo ya mechi hiyo huenda yakazidi kuongeza presha katika vita ya kusaka ubingwa badala ya kupunguza kwa timu moja.

Matokeo yoyote yatakayopatikana katika mechi hiyo hayataweza kutegua kitendawili cha ubingwa kama wadau wengi wa soka wanavyoamini.

Timu yoyote itakayoibuka na ushindi, itakuwa na kibarua cha kupata matokeo mazuri zaidi katika mechi mbili zijazo vinginevyo ushindi huo hautakuwa na maana kwa timu husika.

Simba ikiifunga Yanga, itafikisha pointi 62 ambazo haziwezi kutosha kuipa ubingwa na italazimika kuibuka na ushindi katika mechi mbili kati ya nne zilizopo mbele yake dhidi ya Singida United, Ndanda FC, Kagera Sugar na Majimaji FC ili kutwaa ubingwa kwa kuwa itafikisha pointi 68 ambazo Yanga haitazifikia hata ikipata ushindi kwenye mechi zote zilizobaki.

Pointi tatu za mechi ya Yanga endapo itazipata, zinaweza kutokuwa na faida kwa Simba kama itatoka sare kwenye mechi zote ambazo itabakiza au itapoteza tatu kati ya nne zitakazobaki mkononi kwake na inaweza kujikuta ikishuhudia ubingwa ukienda kwa Yanga endapo itashinda mechi itakazobaki nazo.

Endapo Yanga itaifunga Simba, itafikisha pointi 51, lakini bado itakuwa na kibarua cha kuhakikisha inapata ushindi kwenye mechi sita itakazobakiza mkononi huku ikiombea Simba nayo ipoteze pointi katika mechi nne ilizobakiza kutetea ubingwa kwa mara ya nne mfululizo.

Ushindi dhidi ya Simba hautakuwa na faida kwa Yanga ikishindwa kupata matokeo mazuri katika mechi sita itakazobakiza baada ya hapo, lakini hata kama itashinda zote inaweza isipate ubingwa endapo Simba itashinda mechi zote nne itakazobakiza baada ya kucheza na Yanga.

Kama Simba ilivyokuwa na kibarua kigumu kwenye mechi nne itakazobakiza, Yanga nayo ina shughuli pevu kwenye mechi sita zitakazobaki mkononi mwao, baada ya kucheza mechi ya Jumapili kwa kuwa italazimika kucheza na Prisons, Mwadui na Mtibwa Sugar ugenini huku uwanja wa nyumbani ikiwa na kibarua mbele ya Mbao FC, Kagera Sugar na Azam FC.

Mechi nne za mwisho kwenye Ligi Kuu imekuwa na kumbukumbu mbaya kwa Simba, misimu miwili iliyopita na zilichangia kushindwa kutwaa ubingwa mbele ya Yanga.

Katika msimu uliopita, Simba ilikuwa mbele ya Yanga kwa tofauti ya pointi mbili ilipokuwa imebakiza michezo minne kabla ya ligi kumalizika.

Katika mechi hizo nne, ilipata ushindi mechi tatu na kutoka sare moja ambayo iliwafanya wafikiwe na Yanga ambayo ilitwaa ubingwa kwa faida ya tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Msimu 2015/2016 ambao Yanga ilitwaa ubingwa, mechi nne za mwisho zilichangia Simba iliyopitwa kwa pointi 11 na Yanga, kukosa ubingwa ilipocheza dhidi ya Mwadui, Azam, JKT Ruvu na Mtibwa Sugar.

Katika mechi hizo nne, ilishinda moja dhidi ya Mtibwa Sugar ugenini lakini ilifungwa na Mwadui, JKT Ruvu kabla ya kutoka sare na Azam.

Pia matokeo ya Jumapili hayana usalama kwa timu zote kwa kuwa yatafanya pengo la pointi baina yao kubaki lilelile na hesabu za ubingwa zitabaki kwa timu yoyote kati ya hizo.

“Bado nafasi ya kutwaa ubingwa kwetu ipo iwapo tutapata ushindi kwenye mechi zetu tulizobakiza. Ni kweli Simba wametutangulia kwa pointi lakini pia wamecheza mechi nyingi zaidi yetu jambo ambalo ni faida kwetu,” alisema kocha msaidizi Yanga Shedrack Nsajigwa.

Kocha wa Simba, Pierre Lechantre alisema bado mbio za ubingwa ni ngumu kutokana na ushindani uliopo katika mechi za mwishoni.

“Hakuna mechi rahisi katika kipindi hiki kila timu haitaki kupoteza pointi ndio maana najitahidi kuhakikisha wachezaji wangu wanakuwa fiti kukabiliana na mbinu zozote ambazo timu pinzani zitakuja nazo, lakini nimekuwa nikizifuatilia kwa ukaribu timu zote ambazo tutacheza nazo.

Nafahamu umuhimu wa mchezo dhidi ya Yanga na tayari nimeshaona ubora na udhaifu wao ambao tutafanyia kazi ili tuweze kupata ushindi,”alisema Lechantre.

Wasikie Mwameja, Mayay

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema mechi hiyo ni 50 kwa 50 ingawa mazingira ya mechi yanatoa nafasi kwa Simba kutokucheza kwa presha kama Yanga.

Kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Mohammed Mwameja alisema kuwa mchezo huo utaamuliwa na Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya.