Friday, October 13, 2017

Ubora wa kikosi waipa Simba pointi tatu

 

By Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Achana na suluhu iliyopata dhidi ya Yanga, kikosi cha Mtibwa Sugar kimetabiriwa kipigo katika mchezo wao wa Jumapili mbele ya vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Simba

Mtibwa Sugar inatarajiwa kuwasili jijini kesho kwa ajili ya mechi hiyo dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Uhuru ikiwa na kumbukumbu ya suluhu na Yanga.

Mshindi katika mchezo huo ataongoza usukani wa Ligi Kuu kutokana na timu hizo kulingana pointi zote zikiwa na pointi 11, sawa na ilizonazo Azam FC, lakini Simba inaongoza kwa idadi ya mabao.

Mchambuzi wa soka, Jeff Leah aliitabiria Mtibwa ‘kifo’ katika mchezo huo, huku akifafanua kuwa ubora wa kikosi cha Simba utaipa matokeo timu hiyo ya Msimbazi.

“Bado Mtibwa hawaonekani kuimarika kwenye mechi za ugenini, hata ilivyocheza na Yanga pamoja na kwamba walitoka sare, lakini Yanga ilikuwa na nafasi kubwa ya kushinda.

“Kwenye mechi na Simba, Mtibwa ina wakati mgumu sio tu kushinda bali hata kupata sare kutoka na ubora wa kikosi hicho msimu huu lakini pia inacheza nyumbani,” alisema.

Hata hivyo, makocha wa timu zote mbili kwa nyakati tofauti kila mmoja amekuwa akijinasibu kuondoka na pointi tatu kwa ajili ya kuendelea kusaka ubingwa.

Kocha wa Mtibwa,
Zuber Katwila alisema wamekuja Dar es Salaam kuchukua pointi na kamwe hawataki kuharibu rekodi yao ya kutofungwa, ambayo wameiweka katika mechi tano walizocheza hadi sasa. “Ni hali nzuri kuona kwamba hadi sasa hatujapoteza mchezo, hilo tunataka kuendelea nalo katika mchezo ujao dhidi ya Simba, tunajua ni mechi ngumu lakini tunahitaji ushindi,” alisema Katwila.

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema wanaiheshimu Mtibwa, lakini msimu huu kila mechi kwao ni fainali ambayo wanahitajikushinda ili kutimiza malengo yao na kusisitizakwamba ndivyo itakuwa Jumapili.

“Tumedhamiria kusaka ubingwa kwanguvu zote msimu huu, tunakwenda katika mchezo mgumu ambao tunahitaji ushindi, vijana wapo kamili kwa ajili ya hilo.”

-->