Uchovu Gor Mahia kuibeba Yanga

Kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr

Muktasari:

Siku moja kabla ya mchezo huo, Gor Mahia imeingia hofu baada ya kudai inakabiliwa na uchovu wa mashindano ya Kombe la Kagame yaliyomalizika Julai 13 nchini.

Dar es Salaam. Yanga imetua Kenya kwa kishindo na kuibua hofu kwa wapinzani wao Gor Mahia kabla ya kuvaana katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Timu hizo kongwe zitavaana kesho katika mchezo wa raundi ya tatu hatua ya makundi utakaochezwa Uwanja wa Moi Kasarani, Nairobi.

Siku moja kabla ya mchezo huo, Gor Mahia imeingia hofu baada ya kudai inakabiliwa na uchovu wa mashindano ya Kombe la Kagame yaliyomalizika Julai 13 nchini.

Benchi la ufundi la Gor Mahia ambalo awali lilitamba kuwa litaibuka na ushindi kwenye mchezo huo, limeonyesha wasiwasi likidai muda mfupi wa mapumziko unaweza kuwa kikwazo kwao.

Katika mashindano hayo Gor Mahia ilimaliza nafasi ya tatu nyuma ya washindi wa pili Simba na mabingwa Azam.

Kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr aliliambia gazeti hili kuwa mchezo dhidi ya Yanga huenda ukawa mgumu kwao kutokana na wachezaji wake kutopata muda wa kutosha kupumzika kujiandaa mechi za Kombe la Shirikisho.

“Kimsingi sio mechi rahisi kwetu dhidi ya Yanga kwa sababu ukiangalia tuna siku mbili tu za kujiandaa na mchezo huu ambazo sidhani kama tutafanya programu nyingi zaidi ya zile nyepesi za kuweka sawa miili ya wachezaji kabla ya kuingia uwanjani kucheza.

Tumekuwa na michezo mingi mfululizo ambapo ndani ya siku 17 tulicheza mechi tisa za ushindani jambo ambalo limesababisha wachezaji wangu kuchoka,” aliongeza Kerr.

Kocha huyo wa zamani wa Simba, alisema walirejea Nairobi Jumamosi iliyopita na aliwapa wachezaji siku mbili za mapumziko kupunguza uchovu.

“Kama tungepata muda wa kutosha wa mapumziko na maandalizi nadhani Yanga wangekuwa na wakati mgumu sana kwenye mchezo huu,” alidai Kerr.

Pia alisema anakabiliwa na changamoto ya safu ya ushambuliaji kutotumia vyema nafasi za mabao walizotengeneza kwenye Kombe la Kagame.

Hata hivyo, alisema ana amini wachezaji wake watapambana kwa kuwa walipata nafasi ya kutengeneza nafasi za mabao kwenye mashindano ya Kombe la Kagame ambazo watatumia kupata matokeo mazuri dhidi ya Yanga.

Kerr aliipa tahadhali Yanga kutofanyia kazi udhaifu wa Gor Mahia waliona kwenye mashindano ya Kombe la Kagame kwa kuwa timu yake itabadilika katika mchezo huo.

“Kama Yanga walikuwa wakitufuatilia kwenye Kombe la Kagame na wakajipa imani tutacheza hivyo dhidi yao watakuwa wanajidanganya. Tutaingia uwanjani kushindana ili kupata matokeo mazuri natambua mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa Yanga ni timu bora,” alisema kocha huyo raia wa Uingereza.

Yanga ilianza mashindano ya Kombe la Shirikisho kwa kuchapwa mabao 4-0 na USM Alger ya Algeria, ilitoka suluhu na Rayon Sports ya Rwanda, mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.