Uefa kutambulisha mshindano mapya ya klabu

Muktasari:

  • Uefa kwa sasa inaendesha mashindano mawili ya ngazi ya klabu ambayo ni Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo hushirikisha mabingwa wa Ligi ya kila nchi na timu nyingine tatu au mbili zilizoshika nafasi za juu kwa kila nchi.

Zurich, Uswisi. Shirikisho la soka barani Ulaya (Uefa), limepanga kutambulisha mashindano ya tatu ya ngazi ya klabu kuanzia msimu wa 2021.

Uefa kwa sasa inaendesha mashindano mawili ya ngazi ya klabu ambayo ni Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo hushirikisha mabingwa wa Ligi ya kila nchi na timu nyingine tatu au mbili zilizoshika nafasi za juu kwa kila nchi.

Mashindano mengine ni yale ya Europa Ligi, ambayo hushirikisha timu zinazofuatia kwa ubora baada ya zile nne au tatu za juu katika Ligi mbali mbali.

Hata hivyo haijawekwa wazi kuwa mashindano hayo mapya yanayotarajiwa kutambulishwa na Uefa yatashirikisha timu zipi na yatachezwa wakati gani.

Hayo yamebnainishwa na bosi wa Chama cha Klabu za soka Ulaya (ECA) Andrea Agnelli, ambaye pia ni mjkumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho la soka Ulaya.

Agnelli ambaye pia ni mwenyekiti wa timu ya Juventus, alisema kuwa kwanza watafanyia marekebisho muundo wa sasa wa mashindano yaliyopo kabla ya kuutangaza mfumo huo mpya, utakapopitishwa katika mkutano mkuu wa Uefa utakaofanyika nchini Dublin, Ireland Desemba mwaka huu.

 “Tunatarajia kutambulisha mashindano mapya ya klabu Ulaya, hii itaongeza timu shiriki kutoka 80 za sasa hadi 96, lakini pia itapunguza timu za Europa Ligi kutoka 48 hadi 32 ili kuwa na uwiano sawa timu za mashindano mapya nazo zitakuwa 32,” alisema Agnelli.