Ujio Rais FIFA, Dk Mwakyembe awatwisha zigo vigogo wa TFF

Muktasari:

  • Dk Mwakyembe alitoa kauli hiyo katika mkutano uliojumuisha viongozi wa michezo na wasanii mjini hapa jana.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe, amesema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeshindwa kutumia vyema fursa ya ujio wa Rais wa FIFA, Gianni Infantino katika sekta ya utalii.

Dk Mwakyembe alitoa kauli hiyo katika mkutano uliojumuisha viongozi wa michezo na wasanii mjini hapa jana.

Waziri huyo alisema kuwa TFF ilishindwa kuandaa mazingira bora kwa Rais huyo wa Shirikisho la Soka Duniani na ujumbe wake.

Waziri huyo alisema shirikisho hilo lilipaswa kuandaa mavazi ya asili ambayo yangeitangaza Tanzania nje ya nchi kupitia ugeni wa FIFA.

“Baada ya sherehe wageni wengi walihitaji mavazi ya asili, lakini nilipowauliza viongozi wa TFF walijibu hawakuandaa kwa kuwa hawakujua kama lingeweza kuhitajika,” alisema Dk Mwakyembe.

Waziri huyo alisema wajasiriamali kutoka Nigeria walitumia fursa hiyo kuwauzia wageni hao fulana na baadhi ya mavazi ya Tanzania.

Wakati huo huo, Dk Mwakyembe amewalaumu viongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA) kushindwa kuibua vipaji vya wanasoka chipukizi kwa sasa.

“Uwanja mnaotegemea hauridhishi, upo kama sehemu ya kuegeshea magari ndio maana hata michezo mingi ya kimataifa inashindikana kuileta hapa ili kutangaza vivutio vya utalii,” alisema Dk Mwakyembe.

Baadhi ya viongozi wa vyama waliohudhulia ni riadha, soka, taekwondo, karate na ngumi.