Ukata wamkimbiza kocha Arusha FC

Muktasari:

  • Kocha wa Arusha FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, Martin Mahimbo ameacha kazi baada ya klabu hiyo kushindwa kumpa mkataba kutokana na ukata. Pia wachezaji watatu wa timu hiyo wameondoka kambini kwa kutolipwa stahiki zao.

Arusha.  Athari ya Ligi Daraja la Kwanza kukosa mdhamini imeanza kuiathiri Arusha FC, baada ya Kocha Martin Mahimbo kuikacha timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Akizungumza jana,  Mahimbo alisema ameacha kazi kwa kuwa klabu hiyo imeshindwa kumpa mkataba kutokana na ukata.

Alisema ameshindwa kuendelea na kazi kwa kuwa hajui hatima yake licha ya kuiongoza Arusha katika mechi mbili dhidi ya Geita Gold Mine na Ruvu Shooting ambapo alivuna pointi mbili.

“Nilifanya usajili kwa baadhi ya wachezaji kuwatoa Dar es Salaam na wengine Arusha na tulianza ligi vizuri ugenini, lakini baada ya kurejea hali ilikuwa ngumu na malalamiko ya wachezaji yalizidi nimeamua kuondoka,” alisema Mahimbo.

Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Frederick Lyimo alisema Mahimbo na wachezaji watatu wameondoka kutokana na kukosa fedha za uendeshaji.

Arusha FC ina pointi tatu baada ya kucheza mechi sita, imefungwa tatu na kutoka suluhu michezo mitatu, katika msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza.