Watanzania ughaibuni wafuta Usimba na Uyanga

Muktasari:

  • Imeelezwa kwamba mashabiki waishio ughaibuni walizipa sapoti timu hizo zilipocheza bila kujali wanashabiki Simba au Yanga.

NYOTA wa zamani wa Simba na Yanga wameonyesha kufurahishwa na mashabiki wa Tanzania waishio ughaibuni wanavyozisapoti timu zao nje ya nchi bila kujali Usimba na Uyanga unaoziangusha timu hizo zikicheza nyumbani.

Frank Kassanga 'Bwalya' na Sylvanus Ibrahim 'Polisi' waliwapongea Watanzania waishio Botswana na Misri walivyoziunga mkono timu za Tanzania katika mechi zao za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho bila ubaguzi kama unaofanywa nchini.

"Waliopo Botswana bila kujali Usumba na Uyanga waliishangilia Yanga na kutoka suluhu ni kama waliopo Misri, bila kujali ni mashabiki wa Yanga, waliunga mkono Simba kwa kujua wanaiwakilisha Tanzania, kama mashabiki wa jijini Dar wangebadilika ingezisaidia timu zetu kwa mechi za nyumbani." alisema Kassanga.

Naye Polisi alisema;

"Wanaoishi Misri na Botswana, wametufumbua macho, kama kweli tumeamua timu zetu zinaposhiriki michuano ya kimataifa, tusiwape nafasi wageni kupata ujasiri kama vile wanacheza nyumbani kwao, tubadilike kwani zinatuangusha."

Hata hivyo, Boniface Pawasa nyota wa zamani wa Simba, alisema kinachowafanya Watanzania wanaoishi nje wawe wazalendo kwa Simba na Yanga, zilipocheza ugenini ni kwa kutoziona siku nyingi, hivyo kuziunga mkono tofauti na waliopo Dar.

"Ila uzalendo wao, unawatia moyo wachezaji kujiona sio wapweke, hii iwe funzo kwa mashabiki waishio Tanzania, kuacha kujipendekeza kwa wageni," alisema Pawasa na kuongeza; "Nyie Wanahabari mna nguvu ya kutoa elimu kwa mashabiki, kujua utaifa ni nini na kujua athari za kuwaunga mkono wageni, kunashusha hadhi ya soka la Tanzania."