Utata waibuka Mbeya City, Yanga

Muktasari:

  • Ilikuwa hivi. Baada ya Ambokile kuumia inadaiwa alikwenda nje ya uwanja kupatiwa matibabu na kocha Ramadhani Nsanzurwimo alifanya mabadiliko na nafasi yake kujazwa na Daniel Joram dakika ya 92.

Tukio la mchezaji wa Mbeya City Eliud Ambokile kurejea uwanjani akiwa ametolewa baada ya kuumia, ni moja ya matukio makubwa yaliyojiri katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya timu hiyo na Yanga.

Ilikuwa hivi. Baada ya Ambokile kuumia inadaiwa alikwenda nje ya uwanja kupatiwa matibabu na kocha Ramadhani Nsanzurwimo alifanya mabadiliko na nafasi yake kujazwa na Daniel Joram dakika ya 92.

Hata hivyo, baada ya Ambokile kupona aliomba kurejea uwanjani na mwamuzi Shomari Lawi wa Kigoma alimruhusu kuingia wakati tayari Joram akiwa ameingia kujaza nafasi ya mshambuliaji huyo.

Tukio hilo liliibua tafrani kwa benchi la ufundi ambapo kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alimvaa mwamuzi wa akiba kulalamikia kitendo hicho.

Pia mashabiki wanaodaiwa kuwa wa Yanga walianzisha tafrani kubwa kabla ya polisi kuingilia kati kuwatuliza wakilalamikia tukio hilo. Katika mchezo wa jana, Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbeya City jijini hapa.

Alipoulizwa kama alifanya mabadiliko kujaza nafasi ya Ambokile, Nsanzurwimo alisema hakumbuki na alimtaka mwandishi wa gazeti hili kuwauliza waamuzi.

Hata hivyo, juhudi za kuwapata waamuzi wa mchezo ziligonga mwamba kwa kuwa muda mfupi baada ya mpira kumalizika walichukuliwa haraka na polisi kuingizwa ndani ya gari na kuondoka eneo la uwanjani.

Akizungumza mjini hapa, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani Yanga, Hussein Nyika, alisema wamekata rufani kupinga matokeo hayo.

Yanga ilikuwa ugenini kwenye Uwanja wa Sokoine ikiwa na matumaini ya kupunguza pengo la pointi baina yao na Simba ambao juzi ilitoka sare ya bao 1-1 na Lipuli mkoani Iringa.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, walicheza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kurejea nchini hivi karibuni kutoka Ethiopia.

Yanga ilifuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika licha ya kufungwa bao 1-0 na Welaytta Dicha, lakini ilisonga mbele kwa ushindi wa mabao 2-1 iliyopata mjini Dar es Salaam.

Matokeo hayo yametoa nafasi kwa Simba kujiwekea mazingira ya kujiamini kutwaa ubingwa, baada ya kuukosa tangu 2012.

Simba imebaki kileleni katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 59 katika michezo 25 iliyocheza ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 48 baada ya kuteremka uwanjani mara 23.

Kasi mchezo ilivyokuwa

Yanga ilipata bao lilifungwa na Rafael Daud dakika ya 57, baada ya kuunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Juma Abdul kufuatia Hassani Mwasapili kumchezea madhambi Juma Mahadhi.

Presha ya Mbeya City langoni mwa Yanga ilizaa matunda dakika ya majeruhi baada ya Idd Selemani kufunga bao kwa mpira wa kichwa.

Vurugu uwanjani

Wakati mchezo ukiendelea vurugu kubwa iliibuka dakika ya 59, baada ya mchezaji wa Mbeya City, Ramadhani Malima kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Lawi kwa kumchezea madhambi Yusuph Mhilu.

Mashabiki wanaosadikiwa kuwa wa Mbeya City walianza kurusha mawe uwanjani ikiwa ni ishara ya kupinga kuamuzi wa mwamuzi huyo.

Mchezo huo ulilazimika kusimama kwa takribani dakika tatu kuwapa nafasi Polisi kuwadhibiti mashabiki hao waliokuwa na jazba.

Kipa wa Yanga Rostand alikwenda kulalamika kwa mwamuzi akidai kurushiwa mawe na mashabiki waliokuwa upande wa Mbeya City.

Mwamuzi huyo alilazimika kwenda langoni mwa Yanga katika eneo la kipa na kuokota mawe matatu na kwenda kuyakabidhi kwa mwamuzi wa akiba.