Wachezaji nyota 12 walivyochomoza VPL

Adam Salamba

Muktasari:

  • Ni chipukizi 12 waliong’ara katika Ligi Kuu inayomalizika Jumatatu, ambao majina yao yameanza kuhusishwa na klabu kubwa kama Yanga, Simba, Azam na Singida United.

Dar es Salaam. Hawakuwa maarufu wakati pazia la Ligi Kuu ya Tanzania Bara lilipofunguliwa mwaka jana; lakini sasa saini zao ni lulu.

Ni chipukizi 12 waliong’ara katika Ligi Kuu inayomalizika Jumatatu, ambao majina yao yameanza kuhusishwa na klabu kubwa kama Yanga, Simba, Azam na Singida United.

Ligi hiyo imemalizika kwa Simba kutwaa ubingwa mapema na kuacha mechi za mwisho zisizokuwa za kupambania kutoshuka daraja kutokuwa na mvuto.

Lakini mmoja wa nyota hao, John Tiber alionyesha umaridadi katika moja ya mechi za kupambana kubaki Ligi Kuu alipofunga moja ya mabao bora na kuchangia kuinusuru Ndanda FC ya Mtwara isishuke daraja.

Alichukua mpira upande wa kulia, akakata uwanja kuelekea katikati kabla ya kugongeana na mwenzake na baadaye kufuata pasi aliyotanguliziwa ndani ya eneo la penati, akamkwepa kipa, kabla ya kutikisa nyavu za juu kwa kiki kali.

Tiber na wenzake wameonekana kuwa moto wa kuotea mbali licha ya umri wao mdogo.

Mbali na Tiber, jina jingine linalozungumzwa sana ni la mshambuliaji wa Lipuli ya Iringa, Adam Salamba, ambaye alistua mashabiki wakati alipofunga bao safi la kuongoza katika mechi dhidi ya Simba iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.

Salamba, ambaye kabla ya mchezo huo alikabidhiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi, alikimbilia mpira mrefu kutoka katikati na kuulinda, kabla ya kumgeuza mlinzi wa Simba na kufunga kirahisi kwa kiki ya mguu wa kushoto.

Kwa ujumla, Salamba amefunga mabao manane akiwa na Stand United na Lipuli anayomalizia msimu, na Yanga imeshafanya juhudi za kumnasa, ingawa Lipuli imekataa kumuachia kwa sasa ikisema kanuni haziruhusu mchezaji mmoja kuchezea klabu tatu katika msimu mmoja.

Orodha ya chipukizi hao pia inamjumuisha Salum Kihimbwa, ambaye viongozi wa Mtibwa Sugar waliona kipaji chake mapema na kumfanya awe mchezaji wa kwanza kusajiliwa na klabu hiyo ya Morogoro msimu huu.

Winga huyo anasifika kutokana na uwezo wake wa kupeleka mashambulizi akitokea pembeni, chenga za kuudhi na kutengeneza nafasi kwa wenzake.

Kama ilivyo kwa Salamba, mshambuliaji wa Mtibwa, Awesu Awesu hakuweza kuonekana mapema hadi alipochomoza katika mechi kubwa dhidi ya Yanga.

Awesu na Kihimbwa wametamba katika safu ya kiungo na kuwafunika nyota wakongwe ambao walitegemewa kufanya vizuri msimu huu. Wawili hao wamekuwa uti wa mgongo kwenye timu zao kutokana na uwezo wao wa kutengeneza nafasi za mabao na kufunga.

Si ajabu kwamba jina la Kihimbwa sasa linahusishwa na klabu kubwa kwa ajili ya msimu huu wa usajili.

“Hizo habari kuwa nahitajika nimekuwa nikizisikia, lakini kwa kweli hadi sasa sijafanya mazungumzo na timu yoyote na hata uongozi wangu haujafanya kitu kama hicho,” alisema Kihimbwa.

“Kwa hiyo akili yangu kwa sasa ni kuisaidia Mtibwa. Kama offer (dau) itakuja mezani, tukaafikiana, labda ndio nitaondoka.”

Katika orodha hiyo yumo Habibu Kiyombo, nyota ambaye mashabiki wa Yanga hawatamsahau baada ya kupachika mabao mawili na kuiongoza Mbao kushinda kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Alifunga bao la kwanza kwa juhudi binafsi, akichukua mpira kutoka kushoto mwa uwanja, akaruka madaruga mawili wakati akikata uwanja kuelekea katikati kabla ya kupiga shuti la umbali wa takriban mita 25 lililomuacha kipa wa Yanga akigaagaa chini.

Ukiacha uwezo binafsi wa wachezaji hao, pacha hatari zaidi ya washambuliaji vijana msimu huu inaonekana kuwa ya Prisons, ikiundwa na Eliuter Mpepo na Mohammed Rashid ambao wastani wa umri wao ni miaka 21.

Kwa pamoja, wawili hao wamefunga zaidi ya nusu ya mabao yote ambayo timu hiyo ya Jeshi la Magereza imefunga msimu huu na hivyo kushikilia nafasi ya nne hadi sasa.

Na sasa, Yanga imeelekeza nguvu zake kwa Rashid, mshambuliaji mwenye hatua ndefu, nguvu na mwepesi.

Klabu ya Majimaji pia imetoa nyota mmoja katika orodha hiyo. Kama kuna mchezaji aliyefanya kazi kubwa msimu huu, basi ni Marcel Boniventure ambaye hadi sasa ameifungia klabu hiyo ya Songea mabao 13, idadi ambayo inakaribia nusu ya mabao yote ambayo Majimaji imefunga katika mechi 29. Timu hiyo imefunga mabao 28.

“Nimefuatwa na viongozi wa timu tofauti kama Azam, Yanga, Simba na Singida na nje ya nchi wakitaka kunisajili,” alisema Boniventure akizungumzia habari za kutakiwa na klabu kubwa.

“Kikubwa kwa sasa nasubiri msimu umalizike ndipo nitafanya uamuzi wa mwisho juu ya wapi nitacheza msimu ujao. Lakini kipaumbele changu cha kwanza ni maslahi mazuri.”

Ukiondoa hao, wengine ni Shabani Iddi ambaye ameifungia Azam mabao manane kati ya 28 iliyofunga hadi sasa na Ambokile Eliud aliyeifungia Mbeya City mabao tisa.

Katika orodha hiyo, yumo pia kipa chipukizi wa Prisons, Aron Kalambo, ambaye akiwa na umri wa miaka 23 ameaminiwa na klabu yake kukaa langoni.

Ameonyesha umahiri wa hali ya juu katika lango la timu hiyo na kuifanya iwe moja ya timu ambazo hazijaruhusu idadi kubwa ya mabao msimu huu.

Kalambo anaonekana kuwa na uwezo mkubwa katika kupanga safu yake ya ulinzi, kuwa na makadirio mazuri na kuokoa mashambulizi ya timu pinzani sambamba, hasa mipira ya krosi ambayo imekuwa tatizo kubwa nchini, na uwezo wa kukabiliana na washambuliaji ana kwa ana.

Si ajabu kwamba Prisons ni timu inayoshika nafasi ya tatu kwa kuruhusu mabao machache baada ya kufungwa mabao 18. Simba na Azam ndizo zinazoongoza zikiwa zimeruhusu mabao 14 kila moja hadi sasa.

Wakati Kalambo akitamba langoni, Abdallah Kheri anatamba katika ngome ya Azam FC, akiibuka kuwa nguzo imara ya timu hiyo ambayo ilikumbwa na majeruhi wengi na pia iliondokewa na nyota wake wengi msimu uliopita, akiwemo mchezaji kiraka Erasto Nyoni.

Kheri mwenye umri wa miaka 22, amekuwa akitumika kama kiraka wa kuziba nafasi ya beki wa kulia au kucheza katikati na hii ni kutokana na uwezo wake wa kutumia akili kukabiliana na washambuliaji wasumbufu.

Akizungumzia kuchomoza kwa chipukizi hao, kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila alisema mafanikio yao yanatoa ishara kwamba wachezaji wadogo wakiaminiwa, wanaweza kutoa mchango mkubwa.

“Kama una mchezaji mzuri hakuna sababu ya kumuweka benchi eti kwa sababu ya umri,” alisema Katwila.

“Mpira ni uleule, kikubwa ni kumuandaa vizuri kisaikolojia mchezaji na kumuamini na ndio maana mimi huwa sioni tatizo kuwapa nafasi vijana.”