Wadhamini wamjadili Manji

Muktasari:

  • Taarifa zaidi ni kwamba Baraza la Wadhamini la Klabu ya Yanga, muda wowote linaweza kutoa tamko zito juu ya hatma ya uongozi wa timu utakaotoa picha halisi ya uongozio.

Dar es Salaam. Kabla ya usiku wa jana Jumatano Yanga kushuka uwanjani na kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0, baraza la wadhamini la klabu hiyo na  kamati ya utendaji, walikutana ghafla na kujadili mambo mbalimbali, lakini kubwa likiwa ni Mwenyekiti wao, Yusuf Manji.

Wadhamini hao chini ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) Kepteni George Mkuchika limekutana naKamati ya Utendaji  pamoja na kupongeza utendaji wao, lakini hoja ya Manji ilijadiliwa zaidi.

Taarifa zaidi ni kwamba baraza hilo, muda wowote linaweza kutoa tamko zito juu ya hatma ya uongozi wa klabu utakaotoa picha halisi ya hali ya uongozi ndani ya Yanga.

Mara baada ya kikao hicho hakuna mjumbe yeyote aliyeweza kuzungumzia kilichojadiliwa huku baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji wakiwasukumia baraza hilo kuongea.

"Tulikuwa na kikao na viongozi wetu ni kawaida kwetu kukutana, kilichojadiliwa ungewauliza wakubwa wetu ndio wenye mamlaka ya kuwaeleza haitakuwa busara tukiwasemea," alisema Hussein Nyika, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji.