Wakala wa Pogba ateta na Juve

Muktasari:

  • Safari ya kiungo nyota wa kimataifa wa Ufaransa, Paul Pogba kurejea Turin, haipo mbali sana kuna uwezekano mkubwa akatua katika dirisha la usajili la Januari, mchezaji huyo amemtuma wakala wake Mino Raiola kuanza mazungumzo na Juventus, ikiwa ni dalili tosha kuwa ataondoka Old Trafford baada ya kuzidi kutofautiana na kocha Jose Mourinho

Paris, Ufaransa. Imefichukua wakala wa kiungo mahiri wa Manchester United, Paul Pogba, Mino Raiola, yupo katika mazungumzo na Juventus kuhakikisha mchezaji huyo anarudi Turin alikoondoka mwaka 2016 na kutua Old Trafford.

Pogba juzi alisafiri hadi jijini Paris, Ufaransa siku moja baada ya kuwekwa benchi Jumapili iliyopita katika mechi ambayo Man United ilicharazwa mabao 3-1 na Liverpool katika mechi ya Ligi Kuu England.

Kiungo huyo aliungana katika matanuzi na kaka zake pacha Mathias na Florentin pamoja na rafiki yake kipenzi ambaye ni mchezaji mwenzake wa zamani wa Juventus, Paulo Dybala.

Akizungumza kuhusu hilo Raiola alisema mchezaji huyo amemwambia anataka kuondoka Old Trafford, katika dirisha dogo la usajili wa Januari hivyo kumuagiza azungumze na Juventus ili iweze kushughulikia uhamisho.

“Kwa sasa Paul anataka kurudi Juventus, ni vigumu kwake kuendelea kubaki Man United kwa sababu haaminiwi tena na kocha Jose Mourinho,” alisema Raiola.

Kiungo huyo kwa muda mrefu amekuwa katika malumbano na Mourinho akishutumiwa kucheza chini ya kiwango na hatima yake ndani ya timu haieleweki, ingawa pia kuna tetesi kuwa kocha huyo atatimuliwa kabla ya Krismas.