Wasemavyo makocha klabu za Ligi Kuu

Muktasari:

  • Ligi hiyo ilizinduliwa na mechi ya Simba na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mechi ya Ngao ya Jamii.

Dar es Salaam. Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018/19 unaanza kesho kwa timu mbalimbali kushuka uwanjani kuanza kazi ya kuinyang’anya Simba ubingwa.

Ligi hiyo ilizinduliwa na mechi ya Simba na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mechi ya Ngao ya Jamii.

Hata hivyo, ligi hiyo inaanza ikiwa na changamoto nyingi ikiwemo kukosekana kwa wadhamini.

Gazeti hili lilizungumza na makocha wa klabu mbalimbali za ligi hiyo kusikia maoni na mtazamo wao.

PATRICK AUSSEMS, SIMBA

Ameanza kwa kutwaa Ngao ya Jamii na ni msimu wake wa kwanza kuifundisha Simba, Mbelgiji huyo ana kauli za kishujaa baada ya kudai kuwa amekinoa kikosi chake kikamilifu na kuwaambia wadau wa soka nchini wajiandae kuona burudani ya kutosha kutoka kwa mastaa wake.

“Najisikia vizuri kufundisha klabu kubwa ya Simba, kikosi changu ni kipana na kipo imara,ambacho kitafanya kazi yenye mvuto ya kutetea ubingwa wa ligi hiyo,” anasema.

HITIMANA THIERY-BIASHARA UTD

“Tunajua sisi ni wageni wa ligi lakini hatupaswi kuwa na hofu.Tunaziheshimu timu zote ambazo ziko kwenye ligi miaka mingi lakini hatuziogopi” anasema Thiery

ALLY BIZIMUNGU-MWADUI

“Nimesoma alama za nyakati kutokana na msimu ujao kuwa na mechi 38, ambazo zimetokana na uwezo wa timu 20 ligi kuu, ndio maana kikosi changu nimeamua kujaza vijana, naamini watafanya makubwa kupitia maandalizi niliyowaandaa,”anasema.

MWINYI ZAHERA-YANGA

“Pamoja na changamoto za mtikisiko wa uchumi unaoisumbua Yanga, nitapambana kuhakikisha wachezaji hawaharibikiwi kisaikolojia, badala yake nitawapa mtazamo wa kuwania ubingwa.

“Kikosi kipo imara kwa ushindani wa Ligi Kuu, nimeendelea kuifuatilia kwa ukaribu Mtibwa Sugar, tunayofungua nayo dimba, nimegundua ina ushindani wa hali ya juu ila kwa kikosi changu natarajia ushindi,”anasema.

MBWANA MAKATA-ALLIANCE

“Soka ni mchezo wa wazi, ninaamini wadau wa soka wataona burudani na ushindani kutoka timu yetu ya Alliance, tumejiandaa vizuri na tupo tayari kwa kazi,” anasema Makata.

ATHUMAN BILALI ‘BILO’ -STAND

“Msimu huu kitaeleweka, tuna timu ya kuwania ubingwa na sio kujinasua kushuka daraja, kama tutakwama sana ni kumaliza nafasi ya nne, kwani kikosi kipo safi tayari kwa kuanza kazi,”anasema.

HEMED MOROCCO-SINGIDA UNITED

“Ninakiamini kikosi changu kwamba kitafanya kazi nzuri kutokana na maandalizi tuliyoyafanya, pia wachezaji wanacheza kwa kuelewana kwa maana ya kombinesheni yao ipo vizuri,” anasema.

AMRI SAID-MBAO

“Tumefanya maandalizi ya kutosha, wachezaji wangu wapo tayari kuanza Ligi Kuu ya msimu huu kwa ushindani wa hali ya juu, ninaamini Watanzania wataona mpira wa burudani, lakini wenye manufaa kwa timu yetu kupambania nafasi tatu za juu,” anasema Amri Said.

ZUBER KATWILA-MTIBWA

“Mtibwa Sugar ni chuo cha soka, tutaendeleza utamaduni wetu wa kucheza soka la ushindani, malengo yetu ni kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara,”kauli ya kishujaa kutoka kwa kocha wa Mtibwa Sugar Katwila.

BAKARI SHIME-JKT TANZANIA

“Nimejiandaa kikamilifu kwa maana ya wachezaji kukaa kwa pamoja muda mrefu, najua ligi itakuwa na ushindani mkali, ila naamini kikosi changu kitakuwa mwiba dhidi ya wapinzani wetu,” anasema.

ABDALLAH MOHAMED- PRISONS

“Ninahitaji kusogea nafasi za juu zaidi na sio kushuka chini, nimejipanga kwa ushindani, ninaamini tutakuwa na msimu wa mafanikio,” anasema Mohamed.

HANS PLUIJM-AZAM FC

“Nina wachezaji wa kutosha ambao wana uwezo wa kuipigania timu kufikia malengo tuliojipangia, kutokana na maandalizi tuliofanya na tumecheza mechi mbalimbali za kujipima ubavu,”anasema.

RAMADHAN NSANZURWIMO-MBEYA CITY

“Ligi itakuwa na ushindani mkali,lakini kikosi changu kipo tayari kwa kuonyesha ushindani wa hali ya juu dhidi ya timu pinzani.”

MALALE HAMSINI-NDANDA FC

“Utakuwa ni msimu wa aina yake, kwanza mechi nyingi zitawafanya wachezaji wapate uzoefu,lakini pia maandalizi ya timu yangu yapo vizuri nina kikosi ambacho kitaonyesha ushindani mkubwa dhidi ya wapinzani wetu katika kuwania taji la ubingwa kwa msimu wa 2018/19,’anasema.

SELEMAN MATOLA-LIPULI

“Ninafahamu ligi itakuwa ya ushindani wa hali ya juu, pia inatoa nafasi kwa wachezaji kupata uzoefu kutokana na ujio wa timu nne utakaofanya mechi ziwe 38 badala ya 30, hivyo natarajia kuona vipaji vikubwa, lakini kubwa zaidi timu yangu kushindania ubingwa,”anasema.

ETIENE NDAYIRAGIJE-KMC

“Najua ugumu wa ligi kwani tayari nazifahamu timu nyingi.Licha ya kwamba timu yangu ni ngeni kwenye ligi lakini hilo halitufanyi kuhofia bali tunahitaji kupamnbana ili kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea.”

ABDULMUTIC HAJI - RUVU

“Tumejipanga kushangaza msimu huu kwani tumefanya maandalizi mazuri kuhakikisha tunacheza katika ubora mkubwa na kumaliza ligi katika nafasi nne za juu,”alisema.

MECKY MAXIME- KAGERA SUGAR

“Ukiangalia msimu uliopita hatukufanya vizuri na ilibidi kutumia nguvu kubwa kwenye baadhi ya mechi za mwisho mwisho za mzunguko wa pili ili kuhakikisha tunajinasua na janga la kushuka daraja, lakini safari hii tumejipanga.”