Watoto wamlilia Neymar Brazil ikijifua

Muktasari:

  • Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wakiwemo watoto walibubujikwa machozi baada ya kushindwa kushuhudia mazoezi kutokana na msongamano.

Rio de Janeiro, Brazil. Mamia ya mashabiki wa Brazil wakiwemo watoto, wamejitokeza kushuhudia mazoezi ya timu ya Taifa inayojiandaa na fainali za Kombe la Dunia.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wakiwemo watoto walibubujikwa machozi baada ya kushindwa kushuhudia mazoezi kutokana na msongamano.

Licha ya kubebwa na jamaa, lakini watoto hao walishindwa kumuona Neymar na wenzake waliokuwa wakijifua kujiandaa na fainali hizo zilizopangwa kuanza Juni 14.

Mashabiki wa Brazil wana matumaini timu hiyo itafanya vyema katika fainali hizo wakiwania kombe hilo kwa mara ya sita katika historia ya nchi hiyo.

Neymar aliyerejea uwanjani wiki hii akitokea kwenye maumivu makali ya kifundo cha mguu, alinogesha mazoezi hayo kwenye Uwanja wa Granja Comary mjini Teresopolis.

Baadhi ya mashabiki waliovaa jezi za njano, walivamia geti la uwanja wakilazimisha kuingia, lakini waligonga mwamba kutokana na ulinzi mkali.

Watoto walisaidiwa kubebwa na jamaa zao ili kushuhudia mazoezi hayo lakini waliishia kumwaga chozi, baada ya kushindwa kuwaona kina Neymar. Brazil imepangwa Kundi E.