Waziri Ummy kunogesha mbio marathoni

Muktasari:

  • Mbio za Mbezi Fun Run, zinatarajiwa kufanyika Desemba Mosi na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Dar es Salaam.Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mbio za Mbezi Fun Run, Desemba Mosi, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam, mratibu wa mbio hizo, Omari Kimbau alisema mbio hizo zitashirikisha wakimbiaji wa nusu marathoni kilomita 21, 10 na tano.

Kimbau alisema wanatarajia mbio hizo zitashirikisha wakimbiaji mbalimbali wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani.

Alisema lengo la mbio hizo ni kuimarisha afya, kujenga umoja, mshikamano na amani kwa wakazi wa Mbezi na Dar es Salaam.

Alisema wanatarajia Ummy kuongoza mbio hizo zitakazoanzia na kumalizikia kwenye fukwe ya wazi iliyopo jirani na Lamada, Mbezi Beach.

 

Mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi, Christina Manogi ‘Sinta’ alisema mbali na kukimbia, washiriki pia watapata fursa ya kufanya usafi kwenye fukwe hiyo, kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa hiari na kuchangia damu.

"Maandalizi yanakwenda vizuri na mimi nitakuwa miongoni mwa wakimbiaji wa kilomita 21," alisema Sinta ambaye ni msanii nyota wa zamani wa maigizo.