Wenger ampeleka Sanchez Man United

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo Mchile tangu mwanzo wa msimu huu amekuwa akihusishwa na kutaka kuondoka Arsenal

Baada ya mvutano wa muda mrefu, hatimaye ndoto ya Alexis Sanchez kuondoka Arsenal zinatarajiwa kutimia ndani ya saa 24 zijazo.

Sanchez amekuwa na mzozo wa muda mrefu akitaka kuhama, lakini kocha Arsene Wenger alikuwa akimuwekea ngumu kabla ya jana kukata mzizi wa fitina.

Wenger amesema muda mfupi ujao mchezaji huyo wa kimataifa wa Chile atakuwa mali ya Man United inayonolewa na kocha Jose Mourinho kwa Pauni35 milioni.

Uhamisho wa kutua Man United unaweza kuiduwa dunia kwa kuwa Sanchez alikuwa na ndoto ya kucheza Man City muda mrefu akitaka kuunga na kocha Pep Guardiola.

Kocha wa Man United Jose Mourinho aliingilia kati dili hilo baada ya kuona kocha wa Man City Pep Guardiola, ameshindwa kumngoa makao makuu Etihad kwa mara ya pili.

Mourinho alitamba atamununua Sanchez kwa bei mbaya akitaka kuweka rekodi ya uhamisho England. Mshambuliaji huyo alikuwa kwenye benchi katika mchezo wa juzi waliochapwa mabao 2-1 dhidi ya Bournemouth.

Wenger ameipa nafasi Man United kwa kuwa atafaidika na usajili wa kiungo wa timu hiyo Henrikh Mkhitaryan ambaye amekosa namba katika kikosi cha kwanza.

“Alex angecheza, lakini ni ngumu kwa kuwa yuko katika kipindi kigumu ingawa siku zote amekuwa akijituma, lakini anaweza kuondoka leo. Saa 48 (24) zijazo zitaamua hatima yake,”alisema Wenger.

Kocha huyo alisema mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona hawezi kucheza katika mazingira ya sasa kwa kuwa ana presha ya kutaka kujiunga na klabu nyingine.

Mkhitaryan, alijiunga na Man United kutoka Borussia Dortmund kwa Pauni 30 mwaka 2016 na amekuwa kipenzi cha mkufunzi mpya wa Arsenal Sven Mislintat, tangu akiwa Dortmund.

Arsenal imeanza mchakato wa kutaka saini ya kiungo wa pembeni wa Brazil Malcolm kutoka Bordeaux aliyewekwa sokoni kwa Pauni35 milioni.