Thursday, October 19, 2017

Fusso awaahidi ubingwa mashabiki Tabora

 

Tabora. Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa “Fusso” amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaahadi kutetea ubingwa wao msimu huu.

 Yanga ipo mjini Tabora ikijiandaa na mchezo wake dhidi ya Stand United utakaopigwa Jumapili ijayo mjini Shinyanga.

Juzi timu hiyo ilitoka suluhu na Rhino Rangers katika mchezo wa kujipima nguvu uliopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Fusso alisema awaangalia mchezo moja moja  wa Ligi Kuu kwani wao kila mchezo kwao ni muhimu katika safari yao ya kutetea ubingwa.

“Siwezi kuzungumzia mchezo mmoja wa Stand United na wakati tuna mechi nyingi tu za Ligi Kuu hivyo sisi tumejipanga kushinda mechi zote ili malengo tuliyojipangia yatimie,”alisema Fusso.

Alisema mashabiki wa soka wasipate hofu kwani chama lao lina wachezaji wazuri  wenye kiwango kikubwa ambao wataweza kutetea ubingwa msimu huu.

“Tumejipanga imara tuna wachezaji wazuri na wenye morali hivyo tuko katika mapambano  na mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi tutabeba tena Kombe”alisema Kocha huyo Msaidizi.

Yanga ina pointi 12 ikiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu mpaka sasa.

 

-->