Yanga SC yataka kukwea kilele, Simba kurudisha heshima

Muktasari:

  • Kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga itaikaribisha Singida United, huku watani zao Simba, wakikaribishwa na Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga na mechi hizo zote mbili zitabeba hisia za mashabiki nchini.

Dar/Shinyanga. Yanga leo inapigania kuishusha Mbao FC ya Mwanza na kukaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mabingwa watetezi wa Ligi hiyo, Simba ya Dar es Salaam, itakuwa ikipambana kurejesha heshima yake.

Kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga itaikaribisha Singida United, huku watani zao Simba, wakikaribishwa na Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga na mechi hizo zote mbili zitabeba hisia za mashabiki nchini.

Yanga ambayo hadi sasa haijapoteza mchezo hata mmoja, ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa kwa michezo mitatu, huku Mbao iliyo kileleni ikiwa imecheza michezo mitano na iwapo leo itaibuka na ushindi bila shaka wanajangwani hao watapanda hadi kileleni kwa kufikisha pointi 12, ikiwa na mchezo mkononi. Hata hivyo, timu hiyo inashuka dimbani huku ikiwa na kumbukumbu ya kung’olewa na Singida United kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti.

Katika mchezo wa leo, Yanga itamkosa nahodha wake Kelvin Yondani, ambaye anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano, lakini habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo ni kuwa beki wa pembeni kulia Juma Abdul anarejea uwanjani baada ya kuwa majeruhi kwa muda na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ atakuwepo.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema lazima wapambane ili kushinda mchezo huo wa leo ili waendeleze mwanzo wao mzuri na kujihakikishia kukaa kileleni, huku Kocha wa Singida United, Hemed Morocco naye akisema kuwa wamejiwekea mikakati ya kuondoka na pointi zote tatu leo.

Mwadui vs Simba

Kwa upande wa pili kipigo cha bao 1-0 ilichokipata Simba katika mchezo uliopita kutoka kwa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza, kiliiharibia timu hiyo na kuinyima fursa ya kukaa kileleni, hivyo leo ‘Mnyama’ atashuka dimbani kwa lengo moja la kupata ushindi.

Simba ambayo ilianza kutetereka mjini Mtwara ilipolazimishwa sare na Ndanda FC, leo itashuka kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, ikihitaji ushindi ili kuthibitisha kuwa iliteleza katika mechi mbili za ugenini zilizopita.

Pia Simba inahitaji ushindi kwa udi na uvumba dhidi ya wenyeji wao Mwadui, ili kutuliza hasira za mashabiki wake waliokerwa na matokeo ya mechi mbili zilizopita hasa ile ya kipigo kutoka kwa MBao.

Wengi wanasubiri kuona iwapo Kocha wa Simba, Patrick Aussems amepata jawabu la kutopata matokeo katika mechi mbili zilizopita ama ataendelea kukubali unyonge kwenye mechi za ugenini ambazo zimeonekana kuwa ngumu kwa Simba katika miaka ya hivi karibuni. Akizungumzia mchezo uliopita, Aussems alisema walipoteza kutokana na kutokuwa makini, kwani walitengeneza nafasi na uwanja ulikuwa mzuri lakini hawakupata bao.

“Matokeo ya mchezo uliopita hayakuwa mazuri kwetu ila hatupaswi kutazama nyuma, tunaingia kwa tahadhari ili tupate ushindi, nakiri kuwa Mwanza uwanja ulikuwa mzuri na tulipata nafasi nyingi ila umakini ulikosekana, nimezungumza na wachezaji wangu juu ya hilo naamini leo watakuwa makini,” alisema.

Mapokezi yao Shinyanga

Simba waliingia mjini Shinyanga juzi wakitokea Mwanza ambapo kabla hata ya kufika mjini walikutana na changamoto ya zomea zomea kutoka kwa mashabiki waliodaiwa kuwa ni wa wapinzani wao Mwadui.

Simba walipofika njia panda ya kwenda Mwadui walikuta mashabiki wengi wanaoaminika kuwa ni wa Mwadui ambao walisemekena kujiandaa kuufanyia vurugu msafara wa Simba ingawa waliwadhiti. Hata hivyo kitendo hicho cha mashabiki kimeshutumiwa na kukemewa na Kocha wa Mwadui, Ally Bizimungu ambaye naye alikuwa akienda kufanya mazoezi na vijana wake kwenye uwanja wa Kambarage na kukuta vurugu hizo zikiendelea.

Baada ya Simba kufika hotelini hawakufanya mazoezi ya jioni lakini kocha Aussems na msaidizi wake wa viungo walikwenda kuangalia hali ya Uwanja wa Kambarage ambako Mwadui walikuwa wakifanya mazoezi na kuwaangalia.

Akizungumzia tukio hilo, Bizimungu raia wa Burundi, alisema hajafurahishwa na vitendo vyote vilivyofanywa na mashabiki hao bila kujali ni wa timu gani kwani katika mchezo wa soka hakuna nafasi kwa shabiki kuwafanyia vurugu wachezaji, viongozi wala mashabiki wa timu pinzani.