VIDEO-Hiki ndicho kilichoiua Yanga kwa Rollers

Muktasari:

  • Katika mechi ya marudiano wanatakiwa watambue kwamba upande wa Sikhala ndio upande pekee ambao unategemewa katika kupeleka mashambulizi

 

UBAO wa matokeo tayari unasoma kwamba klabu ya Yanga imefungwa 2-1 dhidi ya Township Rollers, lakini katika mchezo huo kwa jinsi ambavyo ulikuwa unaonyesha kabisa kwamba kulikuwa na makosa madogo madogo yaliyoifanya Yanga kupoteza, lakini pia Township kufanya vizuri.

Mwanaspoti kwa umakini zaidi ilijaribu kuangalia mchezo huo na kugundua baadhi ya matatizo ambayo walikuwa nayo Yanga, lakini pia jinsi ambavyo Township Rollers waliweza kutumia makosa ya Yanga.

KIPA

Ni kijana mdogo ambaye bado anapewa ukomavu katika kikosi hicho, inawezekana makosa madogo madogo ambayo alikuwa nayo Youthe Rostand, ndiyo yalimfanya asianze katika kikosi kile.

Kabwili alionkena kutojiamini katika mechi ile, lakini pia spidi ambayo walikuwa nayo washambuliaji wa Township Rollers, ilionekana kumchanganya.

Goli la kwanza ambalo alifungwa chipukizi huyu, Lemponye kabla hajapokea mpira aliweza kumchungulia na baada ya kuona ametokea aliweza kupiga shuti la juu lililomshinda Kabwili kuufikia mpira.

Katika michezo miwili ya mwisho katika ligi, Rostand ndiye aliyekuwa golini, inawezekana katika mazoezi hakuwa vizuri lakini uwepo kwa Beno Kakolanya ambaye alikuwa akisafiri na timu na kufanya nao mazoezi, inawezekana ulikuwa muda wake sahihi wa kucheza, lakini hakuonekana kuaminiwa katika kikosi hicho kutokana na kukosa utimamu wa mwili (Match Fitness).

MABEKI

Safu ya ulinzi hasa katika upande wa kati, kulikuwa hakuna maelewano katika dakika takribani kumi 10 za mwanzo, kati ya Kelvin Yondani na Said Makapu.

Utulivu haukuwa mzuri sana hasa kwa Said Makapu ambaye alikuwa akisumbuliwa na Lemponye Tshireletso, ambaye ndie alifungua ukurasa wa mabao katika kikosi hicho cha Township Rollers.

Katika upande wa kushoto wa Yanga, Gadiel Michael, alikuwa hapandi kupiga krosi kama ambavyo alikuwa akifanya katika michezo ya nyuma, baada ya Motsholetsi Sikele kumsumbua vilivyo Gadiel.

Sikele alikuwa na uwezo wa kukimbia na mpira kwa umbali mrefu, lakini uwezo wake wa kukaa na mpira na kuufanya anavyoweza, aliweza kuwalazimisha Yanga kufanya mabadiliko ya kiuchezaji.

Yanga ililazimika kumchukua Emmanuel Martin aliyekuwa anacheza winga ya kulia na kuelekea katika winga ya kushoto, ambapo alikuwa anacheza hasa Ibrahim Ajib, kasha Ajib akaenda kucheza kama mshambuliaji, halafu Pius Buswita alienda kucheza kama winga wa kulia, mabadiliko hayo yalionekana kuwa na tija kwani Ukabaji wa Martin kusaidiana na Gadiel ulipunguza spidi ya Sikhele na kumfanya Gadiel apande na kupiga krosi.

Katika mechi ya marudiano wanatakiwa watambue kwamba upande wa Sikhala ndio upande pekee ambao unategemewa katika kupeleka mashambulizi, kutokana na spidi yake pamoja na uwezo wake wa kumiliki mpira na krosi, hivyo watafute mbinu mbadala kama ambavyo walifanya baada ya kumpeleka Martin katika upande ule, kwani hata walivyomtoa na kuingia Mwashiuya, ndio kama walimkaribisha tena Sikhala kwani Mwashiuya alikuwa hashuki chini kuja kukaba kama ilivyokuwa kwa Martin.

WASHAMBULIAJI

Katika safu ya ushambuliaji Yanga, bado kunaonekana kuna tatizo, katika kuhakikisha wanapata bao, bado hawana mtu sahihi wa kuwafungia mabao yao.

Buswita alianza kucheza kama mshambuliaji, aliweza kudhibitiwa na mabeki wa Township, Mosha Gaolalowe na Simisan Mathumo, ambao walionekana kucheza kwa mawasiliano mazuri.

Walipomsogeza pembenis Buswita kwenda kucheza katika winga ya kulia aliyokuwa akicheza Martin ambaye alipelekwa upande wa kushoto, hesabu hiyo ilizaa matunda kwasababu Yanga walianza kushambulia kwa kutumia pande zote mbili.

Tatizo likaja kwa Ibrahim ajib, ambaye alikuja kusimamishwa kama mshambuliaji namba moja, staili yake ya kusubilia mipira ilimfanya Obrey Chirwa ashuke chini kabisa karibu na goli lao kuchukua mpira na kusogeza golini.

Kama Chirwa angekuwa anapelekewa mipira inayovuka dimba la kati, ingekuwa rahisi kwa Ajib kucheza lakini kutokana na uzito uliokuwa umejitokeza ilimlazimu Chirwa kuanza kuchukua mipira chini na kupeleka juu, hata hivyo kutokana na kasi yake pamoja na nguvu yake alikuwa akiisumbua safu ya ulinzi ya Township Rollers.

Urejeo wa Donald Ngoma katika kikosi hicho, kama akifanikiwa kupata nafasi ya kucheza kunaweza kukatengeneza kitu kingine kipya kwake na timu kutokana na aina yake ya uchezaji, hivyo tusubili tuone ni jinsi gani ambavyo Ngoma anaendelea akiwa na wenzake.

KIUNGO

Safu ya kiungo iliyokuwa ikichezwa na Pato Ngonyani pamoja na Papy Tshishimbi, katika dakika za mwanzo ilionekana kama inaendena na kasi ya Wabotswana.

Kadri muda ulivyokuwa unaenda Yanga walionekana kuanza kupotea, kwasababu spidi ya viungo wao, Lemponye Tshireletso aliyekuwa amevalia jezi namba mbili (alifunga bao la kwanza), alikuwa anacheza anavyotaka kutokanana viungo wake wakabaji Joel Mogorosi na Kaone Vanderwesthuisen walikuwa wanakaba vilivyo.

Kiungo cha Yanga licha ya kwamba Tshishimbi alikuwa akicheza sana mpira na kutawala katika dimba la kati, katika upande wa ukabaji Pato alikuwa anahitaji msaada baada ya wapinzani wao kuongeza spidi kadri muda ulivyokuwa ukienda.

Kuna kila sababu ya Yanga kuchezesha viungo wawili wakabaji katika mechi ya marudiano na hiyo ni baada ya Township kuonyesha dhahiri sio timu ya kizembe katika kuchezea mpira, kwani hata bao lao la pili lilipatikana baada ya pasi 18, kasha ndio Sikhele aliingia katika dimba na kumfunga Ramadhan Kabwili bao la pili.