Yanga yaifunika APR Uwanja Ndege Shelisheli

Muktasari:

  • Miamba hiyo ya Afrika Mashariki ipo visiwani humo kwa ajili ya michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Shelisheli. Wachezaji wa Yanga waligeuka kivituo kwenye Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Shelisheli kulinganisha na wenzao wa APR waliofika pamoja nchini humo.

Yanga na APR zipo hapa Shelisheli kwa ajili ya michezo ya mechi zao za kimataifa dhidi ya timu za St. Louis na Anse Reunion FC.

Jana misafara ya Yanga na APR iligongana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Shelisheli, lakini ule wa Yanga ulionekana kutikisa zaidi kuliko wa APR.

Yanga waliwasili uwanjani hapo saa 9 kasoro kwa muda wa huku na baada ya kutua waliingia sehemu ya ukaguzi walikowakuta APR ambao waliwasili saa chache kabla yao.

Ujio wa Yanga ulionekana kupachangamsha uwanjani hapo na kugeuka kivutio kwa wageni wengine hasa watalii ambao walikoshwa na vituko vya wachezaji wa Yanga.

Wachezaji wa Yanga wakiongozwa na Hassan Kessy, baadhi ya wachezaji walikuwa wakipenya kusogea mbele ya foleni.

Tofauti na APR ambao walionekana kuwa watulivu, nyota wa Yanga walianza kupiga picha kwa kutumia simu zao jambo lililopelekea kuvuta hisia za watu uwanjani hapo waliokusanyika kuwatazama.