Yanga yaipiga bao Simba

Muktasari:

Mohammed Issa amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili.

Dar Salaam. Klabu ya Yanga imeanza kukisuka upya kikosi chake baada ya kumsajili mchezaji hodari wa kiungo kutoka Mtibwa Sugar, Mohammed Issa ‘Banka’.

Mchezaji huyo anayefananishwa na nyota wa zamani wa Yanga, Simba na Taifa Stars, Mohammed Banka, ametia saini mkataba wa miaka miwili.

Yanga imemsajili Banka aliyekuwa akitakiwa na watani wao wa jadi Simba ambao walimtupia ndoano katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwaka huu.

Mchezaji huyo aliwahi kukaririwa akidai kuanza mazungumzo na awali na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya mpango huo kufutika kimya kimya.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Hussein Nyika, aliweka bayana sababu za kumsajili mchezaji huyo akidai ni mchezaji aliyelivutia benchi la ufundi.

Nyika alisema Yanga ilikuwa inasaka mchezaji mwenye uwezo mzuri kama Banka ambaye atakuwa na muunganiko mzuri baina ya safu ya kiungo na ushambuliaji.

Banka alikuwa ni miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha kwanza Mtibwa, lakini hakucheza michezo ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, baada ya kupata majeraha akiwa na Taifa Stars.

Awali, Yanga ilikuwa ikimuwinda kiungo wake wa zamani Hassani Dilunga anayecheza Mtibwa kabla ya kumvutia kasi Banka baada ya mchezaji huyo kuhusishwa na mpango wa kujiunga na watani wao wa jadi Simba.

Banka alisema amejiunga na Yanga akiwa na matarajio ya kucheza kwa kiwango bora katika mechi za mashindano mbalimbali.

“Nimejiunga na Yanga nikiwa na matarajio ya kucheza kwa kiwango bora katika mechi za mashindano mbalimbali,”alisema Banka.

Nyika, alisema baada ya kimya cha muda mrefu Yanga imeanza usajili na itaendelea kusajili wachezaji wenye viwango bora kabla ya dirisha kufungwa Julai 26.

“Usajili kwa upande wa CAF bado unaendelea mpaka mwanzoni mwa mwezi ujao, ifahamike tunasajili kwa ajili ya ligi mashindano ya kimataifa,” alisema Nyika.

Usajili huo umefanyika muda mfupi baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Kuivusha Yanga, Tarimba Abbas kutangaza kujiuzulu wadhifa huo kwa madai ya kutopewa ushirikiano na viongozi wa mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Awali, Tarimba aliyewahi kuwa Rais wa Yanga, alidai kuwa amejiondoa baada ya kushindwa kuungwa mkono na viongozi wa klabu hiyo.