Yanga yampa jeuri kocha Mwadui

Muktasari:

  • Yanga ilichapwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Awesu Awesu na kuipa pointi tatu Mwadui katika mchezo huo.

Klabu ya Mwadui imeweka bayana sababu za kuilaza Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa juzi Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Yanga ilichapwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Awesu Awesu na kuipa pointi tatu Mwadui katika mchezo huo.

Akizungumza mjini hapa jana, kocha wa Mwadui Ally Bizimungu alisema siri ya ushindi ni maandalizi kamambe aliyonya kabla ya mchezo huo.

Bizimungu alisema benchi la ufundi na wachezaji waliweka mkakati wa kuifunga Yanga kwa kufanya mazoezi ya kutosha.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara, walipata ushindi mara ya mwisho Machi 12 waliposhinda mabao 3-1 dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kocha huyo alisema mchezo ulikuwa mgumu, lakini ni faraja Mwadui kupata pointi tatu zilizokuwa katika mpango wao katika mchezo huo.

“Tulijiandaa na kutulia uwanjani lakini tulihitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu,”alisema Awesu.

Mwadui inashika nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 33.

Yanga ambayo imepoteza mechi tano msimu huu, ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 48 baada ya kucheza michezo 27.