Yanga yatolea macho mamilioni CAF

Muktasari:

  • Endapo timu hiyo itafuzu hatua ya makundi itapata Dola 275,000 (Sh milioni 616) zinazotolewa na Caf.

Yanga ina kazi moja tu ya kusaka ushindi dhidi ya Waleytta Dicha ili kujihakikishia kuvuna mamilioni ya CAF kwa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, leo watashuka Uwanja wa Manispaa jijini Hawassa wakiwa na mtaji wa mabao 2-0 waliyopata katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam Aprili 7.

Mbali na kuwania nafasi ya kupenya katika hatua ya makundi, Yanga itavuna Dola 275,000 (Sh616 milioni) zinazotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Siyo Yanga tu itakayofaidika na fedha za CAF hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nayo ina mgawo wake wa asilimia tano kwa kila kiasi kitakachoingia Yanga.

Endapo Yanga itafuzu hatua ya makundi itapata Dola 275,000 (Sh 616milioni ) na kuichangia TFF Dola 13, 750 (Sh30.8milioni).

TFF inategemea kupata mgawo wa Dola 17500 (Sh 39.2milioni), iwapo Yanga itafuzu robo fainali itapata Dola 350,000 (Sh 785milioni).

Kama itafuzu nusu fainali itapata Dola 450,000 (Sh1bilioni) itaichangia TFF Dola 22,500 (Sh 50.4 milioni).

Endapo Yanga itacheza fainali itakapotwaa ubingwa itaingiza Dola 1.25 milioni (Sh2.8bilioni), TFF itavuna Dola 62,500 (Sh 140.1milioni).

Lakini kama Yanga itamaliza nafasi ya pili, TFF itaweka mfukoni Dola 31, 250 (Sh 70milioni) wakati miamba hiyo ya Jangwani itafunga mwaka na Dola 625,000 (Sh1.4bilioni).

Maisha bila Lwandamina

Yanga itamkosa kocha wake George Lwandamina aliyetimkia Zambia na sasa timu hiyo ipo kwenye mikono ya Noel Mwandila na Shadrack Nsajigwa wenye jukumu moja tu la kuthibitisha wanaweza kuvaa viatu hivyo.

Habari njema kwa Yanga katika mchezo huo ni kurejea kwa nyota wake beki kisiki Kelvin Yondani, viungo Said Juma ‘Makapu’, Thabani Kamusoko na mshambuliaji Obrey Chirwa waliokuwa wakitumikia adhabu ya CAF.

Hata hivyo, Yanga itamkosa mshambuliaji Ibrahim Ajibu aliyeachwa Dar es Salaam akidaiwa kuuga ghafla muda mfupi kabla ya safari ya kwenda Ethiopia.

Mchezo huo umekuwa gumzo kwa mashabiki wa soka jijini hapa hasa wakiamini Dicha inaweza kufanya kile ilichofanya dhidi ya Zamalek ya Misri waliposhinda 2-1 na baadaye kuitoa mashindanoni.

Yanga inahitaji sare yoyote au isifungwe zaidi ya bao moja na wenyeji kama inataka kusonga mbele katika mashindano hayo.

Maandalizi Yanga

Ikiwa hapa Yanga ilifanya mazoezi mara mbili juzi na jana jioni chini ya makocha Mzambia Mwandila na Nsajigwa.

Kurejea kwa kina Yondani kumepangua kikosi hicho kama ambavyo ilionekana katika mazoezi ya jana, lakini akikosekana Makapu kwa wachezaji wanaotarajiwa kuanza mchezo huo.

Huenda kipa Youthe Rostand atasimama kwenye milingoti mitatu akilindwa na mabeki Hassani Kessy, Haji Mwinyi, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Yondani.

Katika kiungo wanatarajiwa kuanza Raphael Daud, Pappy Tshishimbi, Pius Buswita, Kamusoko na ushambuliaji yupo kinda Yusuf Mhilu na Chirwa.

Mwandila alisema wako tayari kwa mchezo huo baada ya kumaliza kutengeneza kikosi cha kwanza.

Alisema wanatambua ugumu wa mchezo na amewataka wachezaji kuzingatia nidhamu wakitambua Dicha siyo timu ya kubeza.

“Tunawajua wapinzani wetu sio timu nyepesi, tunawaheshimu lakini tutaingia na mipango yetu kuwapa wakati mgumu na hatutaki kujilinda tutawashambulia kwa tahadhari,”alisema Mwandila.

Dicha ilijichimbia mafichoni tangu iliporejea nchini hapa baada ya kipigo cha mabao 2-0.

Yanga inashiriki Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa na Township Rollers ya Botswana katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa matokeo ya jumla ya mabao 2-1.

Yanga ina historia nzuri kwenye hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika, mwaka 2016 iliitoa Sagrada Esperanca ya Angola na kufuzu hatua ya makundi.

Unyonge Ethiopia

Pamoja na Yanga kuzionea timu za Ethiopia hawajawahi kushinda nchini humo zaidi ni sare mara mbili.

Yanga ilikutana mara ya kwanza na timu ya Ethiopia mwaka 1969, katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa), ilitoa Saint-George kwa jumla ya mabao 5-0.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Ethiopia, timu hizo zilitoka suluhu na mechi ya marudiano Yanga ilishinda 5-0 na kusonga mbele hadi robo fainali.

Yanga ilikutana kwa mara pili na Coffee FC mwaka 1998 na kuitoa kwa jumla ya mabao 3-8, katika hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Ethiopia Coffee FC ililazimisha sare 2-2, ziliporudiana Yanga ilishinda 6-1 nyumbani na kucheza hatua ya makundi.

Katika Kombe la Shirikisho mwaka 2011, Yanga ilitolewa kwa jumla ya mabao 6-4, ilianzia nyumbani na kulazimishwa sare 4-4 na Dedebit kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa marudiano uliochezwa Ethiopia, Dedebit ilichapa Yanga mabao 2-0.