Yanga yatua kibabe Shelisheli, Chirwa aamua kuvunja ukimya

Muktasari:

  • Timu ya Yanga iliondoka nchini jana alfajiri kwenda Shelisheli na imetua salama katika mji mkuu wa nchi hiyo Victoria, tayari kwa kuikabili St Louis, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

 Kitendo cha Yanga kumuacha mshambuliaji nyota Obrey Chirwa katika safari ya kwenda Shelisheli, kimewashitua wadau wengi wa soka nchini.

Timu ya Yanga iliondoka nchini jana alfajiri kwenda Shelisheli na imetua salama katika mji mkuu wa nchi hiyo Victoria, tayari kwa kuikabili St Louis, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kikosi hicho kilipokewa saa tisa alasiri na kupata mapokezi kutoka kwa Watanzania wanaoishi nchini humo na baadhi ya viongozi wa Yanga waliotangulia mapema Shelisheli kuweka mambo sawa.

Baada ya kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, timu hizo zitarudiana keshokutwa.

Chirwa ameachwa kutokana na majeraha ya misuli, lakini ameibua mjadala kuhusu mustakabali wa Yanga katika mchezo huo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Chirwa alisema hakupenda kukosa mchezo huo, lakini afya yake haikumruhusu kusafiri.

“Siko vizuri nina maumivu ya misuli, lakini pamoja na kutosafiri naamini tutasonga mbele na kucheza hatua inayofuata,” alisema Chirwa.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo alisita kueleza mbinu anayodhani ikitumiwa vyema itawavusha salama katika mchezo huo.

Pia alisita kutoa maoni kuhusu mshambuliaji anayeweza kuvaa viatu vyake katika mchezo huo akidai wote ni hodari.

Mbali na Chirwa, wachezaji wengine walioachwa ni Amissi Tambwe, Andrew Vincent ‘Dante’, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Yohana Nkomola.

Adolf, Tino watoa kauli

Wakati Chirwa akiwatuliza mashabiki, nyota wa zamani wa Taifa Stars, Mohammed Rishard ‘Adolf’ alisema Yanga inaweza kushinda licha ya kutokuwepo mchezaji huyo.

“Yanga sio Chirwa kukosekana kwake si tatizo wao kushindwa kusonga mbele, Yanga imesajili kikosi ambacho ni kipana kila aliyesajiliwa ana uwezo wa kucheza,”alisema nguli huyo.

Naye nyota mwingine wa zamani wa Taifa Stars, Peter Tino aliwataka washambuliaji kuongeza kasi na kucheza kwa kujiamini dhidi ya St Louis.

Tino alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwa Yanga kwa kuwa ina mtaji mdogo wa bao la nyumbani, hivyo inatakiwa kucheza kwa nguvu dakika zote tisini.

“Shelisheli watahitaji kuwa salama nyumbani, sio mechi rahisi kwa Yanga, nawasisitiza washambuliaji wasipoteze nafasi wanazopata kufunga,”alisema mshambuliaji huyo wa zamani.

Rekodi

Licha ya Yanga kuanza kwa ushindi kiduchu dhidi ya St Louis, baadhi ya rekodi zinaipa nafasi kuvuka raundi ya awali katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tangu mwaka 1997, Yanga imeshiriki mashindano hayo kwa kuanzia hatua ya awali mara tisa na ilisonga mbele mara tano na kushindwa kuvuka mara nne.

Msimu wa mwaka 2009, Yanga iliitupa nje Etoile d’Or kwa jumla ya mabao 14-1, mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Yanga ilishinda mabao 8-1 na ziliporudiana ilishinda 6-0.

Mwaka 2014 Yanga iliing’oa Komorozine de Domoni kwa mabao 12-2, mchezo wa kwanza ilishinda 7-0 kabla ya kuirarua 5-0 katika mechi ya marudiano.

Miaka miwili baadaye Yanga iliing’oa Cercle de Joachim SC kwa mabao 3-0, lakini safari hii ilianzia ugenini Mauritius iliposhinda bao 1-0 kabla ya kupata ushindi wa mabao 2-0 Dar es Salaam.

Msimu uliopita, Yanga ilianzia hatua ya awali na kuwaondoa Ngaya Club de Mde ya Comoro kwa mabao 6-2, ilishinda ugenini 5-1 na kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani.

Ingawa Yanga ina rekodi nzuri katika mechi za hatua ya awali, mchezaji chipukizi wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa nchini humo, Hussein Kazi alisema Yanga inatakiwa kucheza kwa tahadhari mchezo huo.