Yaya Toure arudi Olympiakos

Muktasari:

  • Kiungo nyota na nahodha wa zamani wa Ivory Coast, Yaya Toure amerejea kwenye klabu yake ya kwanza kuitumikia barani Ulaya ya Olympiakos ya Ugiriki kwa mkataba ambao haujawekwa wazi na  tayari ametambulishwa kwa mashabiki

Athens, Ugiriki. Kiungo nyota wa zamani wa Ivory Coast, Yaya Toure amerejea kwenye klabu yake ya kwanza kuitumikia barani Ulaya ya Olympiakos ya Ugiriki.

Nyota huyo wa zamani wa Barcelona na Manchester City, amesema alipokea ofa kutoka klabu mbali mbali za Ulaya, Asia na Marekani na akazitolea nje akichagua kurudi kwenye klabu hiyo iliyomuibua katika msimu wa mwaka 2005-2006.

Mchezaji huyo mwenye miaka 35, aliandika katika tovuti yake kuwa ametimiza ahadi aliyoiweka mwaka 2006 wakati akiondoka.

“Ni furaha iliyoje leo kwangu kutimiza ahadi yangu niliyoiweka mwaka 2006 wakati naondoka hapa,” alisema.

Alisema hahitaji kutoa ahadi nyingi kwa maneno bali ataiachia miguu yake iweze kuelezea amerudi na nini maalumu kwa mashabiki wa klabu hiyo, ingawa kikubwa ataipa mataji.

“Nina kiu cha mafanikio hasa ya mataji kama nilivyokuwa hapa wakati nachipukia katika soka, ninafurahi kukutana tena na mashabiki wa klabu hii ya Olympiacos,” alisema.

Alisema anaifahamu vizuri Ligi kuu ya Ugiriki na ushindani ulivyo anaamini anacho kitu cha kuchangia katika mafanikio ya klabu yake.

Hata hivyo siyo Toure wala klabu hiyo iliyobainisha kiasi cha fedha kilichotumika kwa usajili wala mshahara atakaolipwa lakini vyanzo vya ndani vimedai kuwa atalipwa Euro 2.5 milioni kwa msimu sawa na Dola za Marekani 2.9 milioni.

Mchezaji huyo alitambulishwa kwa mashabiki wa Olympiacos juzi Jumapili baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Ugiriki dhidi ya PAS Giannina wakishinda kwa mabao 5-0.

Toure aliyeipa Man City mataji matatu ya Ligi Kuu England, mawili ya Kombe la Ligi na moja la FA katika miaka minane aliyoitumikia, alitwaa pia taji la Ligi Kuu Hispania, Kombe la Mfalme na Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Barcelona.

Anatarajiwa kuiongezea nguvu timu yake ambayo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya tatu ikiwa ni nafasi ya chini kuwahi kushikwa na klabu hiyo kwa miaka 23 iliyopita, imetwaa ubingwa mara 20 katika miaka 22.

Timu hiyo imefuzu kwenye michuano ya Europa Ligi baada ya kuichapa Burnley ya England kwa jumla ya mabao 4-2 katika mchezo wa mtoano kuwania nafasi hiyo.