Kili Stars yaendeleza uteja kwa Z’bar

Muktasari:

Timu hiyo ya visiwani inasaka ubingwa wa pili wa Kombe la Chalenji tangu ilipofanya hivyo 1995.

Nairobi. Zanzibar Heroes imeendelea kutakata katika  mashindano ya Kombe la Chalenji baada ya kuichapa Kilimanjaro Stars kwa  mabao 2-1 kwenye  Uwanja wa Kenyatta, Machakos.

Mabao ya Zanzibar Heroes yalifungwa na Khasim Suleman na Ibrahim Ahmada wakati lile la Kili Stars lilifungwa na nahodha Himid Mao.

Ushindi huo unaifanya Zanzibar  kuongoza Kundi A ikiwa na pointi sita ikifuatiwa na Kenya yenye pointi nne, Libya ni ya tatu kabla ya mechi yake dhidi ya Rwanda inayoshikilia mkia wakati  Kilimanjaro Stars ikiwa na pointi moja baada ya mechi mbili.

 Kilimanjaro Stars ilipata pigo dakika ya 10 baada ya beki wake Kelvin Yondani kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Boniface Maganga iliyolazimisha safu ya ulinzi kubadika.

Maganga kwenda pembeni na Erasto Nyoni kuingia katikati hali iliyotoa mwanya kwa Zanzibar kupitisha mashambulizi yao kutokea pembeni.

Kilimanjaro Stars  ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 28 lililofungwa na Himid Mao kuipatia kwa shuti kali akimalizia pasi ya Danny Lyanga.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Kili Stars ilikuwa mbele kwa bao 1-0  licha ya kwamba Zanzibar Heroes kuongoza kwa umiliki wa mpira.

Kipindi cha pili timu zote zilirejea kwa kasi, lakini Zanzibar Heroes walifanikiwa kusawazisha bao dakika ya 66 lililofungwa na Khamis Suleiman kwa shuti akimalizia pasi ya Suleima Kassim Selembe.

 Ikionyesha kuwa imepania kushinda mchezo huo, Zanzibar Heroes iliendelea kulishambulia lango la Kilimanjaro Stars kama nyuki na kufanikiwa kupata bao la pili lililofungwa dakika ya 78 na Ibrahim Ahmada aliyeingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya Khamis Suleiman aliyeumia.

Zanzibar sasa inajiandaa na mchezo wake dhidi ya Libya wakati Tanzania Bara itacheza dhidi ya Rwanda katika kuamua hatma yake ya kuendelea na mashindano hayo.