Zahera achekelea sare Azam, KMC

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema sare ya mabao 2-2 waliyopata Azam FC dhidi ya KMC, katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara juzi, imemshusha presha.

Zahera alisema Azam na Simba ndiyo wapinzani wao wakubwa katika mbio za ubingwa, hivyo matokeo kama hayo yanampa faraja.

Azam juzi ilishindwa kuiengua Yanga kileleni baada ya sare hiyo kuifanya ifikishe pointi 40 katika mechi 16 na Yanga imebaki kileleni ikiwa na pointi 41 kwa michezo 15 iliyocheza.

Kocha huyo raia wa DR Congo alisema angependa kuona wachezaji wake wakishinda mechi zote 19 za mzunguko wa kwanza.

“Simba hata ikishinda michezo ya kiporo nitakuwa mbele kwa pointi nne, lakini kwa Azam kazi bado wako vizuri ,” alisema Zahera.

Beki wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ alisema mkakati wao ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu licha ya kupitia kipindi kigumu cha mtikisiko wa kiuchumi ulioikumba klabu hiyo.

Meneja wa Azam FC, Philipo Alando alisema Yanga imegeuka mshindani mkuu wa mbio za ubingwa na kwao sare ya juzi imewatibulia mipango.

Yanga ambayo ilikuwa haipewi nafasi ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu msimu huu kutokana na kutokuwa na kikosi imara, imeanza kuwashitua wengi kutokana na matokeo mazuri inayopata.