Mourinho kuamua hatma ya Zlatan

Muktasari:

Mshambuliaji huyo tangu aliopoumia miezi saba iliyopita ameshindwa kurudi katika ubora wake

London, England. Jose Mourinho ni lazima afanye uamuzi mgumu sasa wa kumuanzisha Zlatan Ibrahimovic katika kikosi chake cha kwanza Manchester United kinachojianda na mechi dhidi ya West Brom leo.

Nyota huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain amecheza dakika 73, zote akiingia akitokea benchi tangu aliporejea baada ya kufanyiwa upasuji wa goti alicheza dhidi ya Newcastle.

Kuna wasiwasi kuwa Ibrahimovic amefikia mwisho baada ya kuumia goti wakati wa mchezo wa robo fainali ya  Europa Ligi dhidi ya Anderlecht mwezi Aprili.

Timu ya madaktari ya Manchester United pamoja na benchi la ufundi wameanza kuwa na wasiwasi huenda staa huyo wa zamani wa Juventus, Inter Milan, AC Milan, Barcelona, Ajax na PSG asirudi tena katika ubora wake.

Kocha Jose Mourinho amewahi kumuacha nje katika mechi mbili tangu kurudi kwake ili aende Gym kwa ajili ya kujiweka fiti zaidi katika eneo ambalo aliumia vibaya goti lake.

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 36, hata hivyo alirejea uwanjani mapema zaidi ya ilivyotegemewa, japokuwa ni wazi kuwa Mourinho angependa kumtumia haraka iwezekanavyo.

Kocha Man United wiki iliyopita alizungumzia kuhusu Ibrahimovic, ambaye bado hajafunga bao lolote tangu arejea, lakini amehusishwa kucheza nafasi ya Lukaku aliyefunga bao Jumatano iliyopita wakati Man United ikichapa Bournemouth kwa bao 1-0 kwenye Uwanja Old Trafford.

"Tutalazimika kufanya mzunguko kwa wachezaji," alisema Mourinho bila kuzungumzia moja kwa moja kuhusu hali ya Lukaku.

"Nitakuwa nabadilisha wachezaji wachache kila mechi, kwa sababu nafikiri ni vigumu kwa mchezaji kucheza mechi zote za Desemba na mwanzoni mwa Januari."