Mbunge Sugu alivyoizungumzia tozo ya Sh5 milioni kwa wasanii

Mbunge wa Mbeya Mjini, (kushoto) Joseph Mbilinyi maarufu Sugu

Moja ya mambo yaliyoibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii wiki moja iliyopita ni pamoja na suala la kanuni mpya ya tozo mbalimbali iliyotangazwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).

Tozo hizo zilitangazwa kupitia ukurasa wake wa Twitter, zilionyesha mabadilko ya viwango mbalimbali kwa wasanii ambavyo vilipaswa kuanza Julai.

Katika tangazo hilo lilionyesha kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha kanuni za Basata za mwaka 2018, gharama za usajili wa wasanii na shughuli nyingine zinaanzia Sh15,000 hadi Sh50,000.

Pia Jedwali la viwango hivyo linaonyesha kuwa gharama zimeanzia Sh20,000 hadi Sh5 milioni ikiwa ni pamoja na kampuni au taasisi zitakazotaka kuandaa matukio ya kibiasahra kutakiwa kuilipa Basata Sh2 milioni kupata kibali wakati yale matukio yasiyo ya kibiashara yenye kiingilio yatalipiwa Sh1.5 milioni.

Vilevile, kwa zile kampuni ambazo zinatumia wasanii kutangaza bidhaa zao kwa kila tukio zinapaswa kulipia Sh5 milioni kwa kila tukio.

Kutokana na tangazo hilo, wasanii mbalimbali walipaza sauti zao kupitia mitandao ya kijamii akiwemo Nikki wa Pili kutoka kundi la Weusi aliyesema kanuni hiyo si rafiki na haikuwashirikisha wadau wa sanaa kabla ya kutangazwa.

Msanii mwingine aliyepinga hilo ni Wabiro Wassira “Wakazi’, ambaye anasema kitendo kilichofanywa na Basata cha kuzibana kampuni ambazo zinafanya kazi na wasanii, ni kutaka sasa zitumie vikaragozi badala ya watu.

Mbaya zaidi Wakazi anasema wanachukua maamuzi hayo huku wakijua si wasanii wote wanaopata matangazo na kampuni kubwa, hivyo kuja na kanuni hizo ni kama kutaka kuwaminya wasanii zaidi katika kujitafutia maisha.

Kauli hizo za kupinga kanuni hizo zinaungwa mkono pia na mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ anayetaka Basata kuwaachia kazi ya kutoza kodi Mamlaka ya Mapato (TRA) na wao wabaki na jukumu lao la kuwalea wasanii kwa madai ndilo lengo la kuanzishwa kwake.

Sugu ambaye pia ni waziri Kivuli wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na msanii wa muziki wa hip hop, anasema anachokiona sasa ni Basata kutoka katika majukumu yake ya msingina kuingilia kazi ambazo zilipaswa kufanywa na TRA, huku ikiacha zake za ulezi wa wasanii.

Mbunge huyo anasema anachoona hadi kufika kuundwa kwa kanuni hizo ni kutokana na watendaji wengi waliopo Basata kuwa si wasanii, hivyo hawana wanalolijua kuhusu changamoto mbalimbali wanazopitia wasanii.

Kutokana na hilo, anasema mambo mengi yamekuwa yakifanywa kwa kukurupuka na kutoa mfano hata suala la kufungia wasanii mara kwa mara si jukumu lao, badala yake kazi hiyo ingepaswa kufanywa na mahakama.

Katika ushauri wake, Sugu anasema ni vyema kabla ya Basata kutangaza kanuni na sheria zozote ikakaa na viongozi wa wasanii kuyajadili mambo hayo badala ya kuyawasilisha wakiwa tayari wameshapitisha, jambo linaloibua manung’uniko ambayo yangeweza kuepukika.

“Nina wasiwasi watu waliopewa jukumu la kuiendesha Basata kama wametoka kwenye sanaa, kwani wamekuwa wakitoka nje ya majukumu yao na walichokifanya cha kuleta kanuni zao hizo sikubaliani nazo, kwani kabla ya kuzifanya ni lazima wawashirikishe wasanii wenyewe kwa upana ukizingatia wana vyama vyao,” anasema.

Kauli ya Serikali

Hata hivyo baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wasanii wengi, waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, Julai 14 alikutana na viongozi wa vyama vya wasanii kujadili suala hilo na kuwapa muda wa kwenda kukaa pamoja ili waje na mrejesho wa nini wangetaka kiboreshwe katika kanuni hizo kabla hazijaanza kutumika.

Hata hivyo, Dk Mwakyembe hakusita kuwalaumu wasanii juu ya tabia zao za kutohuhudhuria vikao pale wanapoitwa katika mikutano mbalimbali na kusubiri kulalamikia sheria zikishapitishwa.

“Pamoja na kwamba nimewapa muda mkangalie namna gani mngependa kanuni hizo ziboreshwe, nawasihi wasanii bila kujali ukubwa wa majina yenu muwe mnahudhuria vikao mnapoitwa kwa kuwa vikao hivyo pia ni muhimu katika kuboresha kazi zenu za kila siku,” alisema waziri huyo.

Pia aliema tozo mbalimbali ambazo ziko katika kanuni hiyo mpya ni katika kuhakikisha wasanii wanafaidika na kazi zao na kwamba, asilimia 50 ya fedha zitakazokusanywa zitaingia katika mfuko wa wasanii ambao wao ndio watakuwa na mamlaka ya kuzitumia watakavyo.