Msondo Ngoma, nyani mzee katikati ya jiji kwa miaka 54

Waswahili wanasema ukiona nyani mzee mjini, ujue amekwepa mishale mingi. Ndivyo ilivyo kwa bendi ya Msondo Ngoma ambayo mwaka huu imetimiza miaka 54 tangu iundwe.

Ndiyo bendi kongwe nchini yenye maskani yake Amana, Ilala jijini Dar es Salaam, lakini iliyoshindwa kuzuia isitimuliwe kufanyia maonyesho Ukumbi wa Amana.

Lakini ni sababu za msingi kuwa ukumbi uko jirani na Hospitali ya Amana ambayo ingependa wagonjwa wasumbuliwe na kelele za muziki usiku.

Kuondolewa Amana ni moja ya mishale ambayo Msongo Ngoma imekwepa tangu ianzishwe. Mishale mingine ni kuporwa wanamuziki na safu nzima ya waimbaji kupoteza maisha.

Pia iliyumbishwa kwa kuhamishwa kutoka Chama cha Wafanyakazi (Nuta) kuwa jumuiya ya Tanu na baadaye CCM, kurudishwa kwenye chama cha wafanyakazi cha Tucta na baadaye OTTU kabla ya kujitoa na baadaye kurudi.

Msondo Ngoma Music Band, inayojulikana zaidi siku hizi kwa nyimbo zilizo kwenye albamu za Rabana, Piga Ua Talaka Utatoa na Ajali, .

Ilianzishwa na Chama cha Wafanyakazi (Nuta) mwaka 1964 na pamoja na misukosuko yote, bado inang’ara, japo haisikiki sana kwenye vyombo vya habari.

Wakati huo ikiitwa Nuta, Msondo ilikuwa bendi iliyotoa hamasa kwa wananchi na kufikisha ujumbe wa viongozi wa Tanu/CCM na serikali.

Nyimbo 10 za kwanza za Nuta Jazz zilirekodiwa Aprili 15, 1967, wimbo wa kwanza ukiwa “Kambona Tanzania”. Wakati huo ilikuwa na wanamuziki kama Hamis Franco (solo gitaa), ambaye inadaiwa alitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kapteni Jonh Simon, Kiiza Hussein (second solo), Ahmad Omary, Selemani Mgogo, Mzee Hamisi Chama (besi), Hamad Omary (rythm) na John Ojungo anayedaiwa kuwa na asili ya Nigeria.

Wengine ni mwimbaji kiongozi Muhidin Maalim Gurumo aliyetoka Kilimanjaro Chacha Band, Abel Baltazar (mwaka 1968 akitokea Kilosa Jazz), na Said Mabera “Dolta” aliyejiunga mwaka 1973.

PANDA SHUKA

Nuta ikasimama na kuwa bendi kipenzi iliyovuta macho ya wengi, wakiwemo waliotaka kumiliki kundi kama hiyo na hivyo kuanza kuwachomoa wanamuzki.

Mwanamuziki wa kwanza mkubwa kuikacha bendi hiyo alikuwa Abel Bartazal aliyejiunga na Dar International mwaka 1977 na baadaye Gurumo aliyengana na Bartazal mwaka 1978 kuanzisha bendi ya Mlimani Park, akiasisi mtindo wa Sikinde Ngoma ya Ukae.

Ikiwa imeshabadilishwa jina na kuwa Juwata, Msondo ikamchukua mpiga solo aliyeibukia kuwa maarufu, Kassim Mponda na mwimbaji mwenye sauti ya chiriku, Belesa Kakele kutoka Vijana Jazz.

Bendi ikaingia kambini Zanzibar na mwaka 1979 ikaibuka na vibao vikali kama vile “Uzuri si Shani”, “Sogea Karibu” na “Kaka Adamu”, nyimbo ambazo zilimng’arisha Hassan Rehani Bitchuka, kiasi cha Mlimani Park haikuchelewa kumng’oa mwaka huo.

Chuo cha mafunzo

Pengo la Bitchuka ‘Stereo’ liliikuwa kubwa kwa Juwata Jazz, lakini haukuwa mwisho kwa Mlimani Park kuchukua wanamuziki kutoka bendi hiyo.

Mwaka huohuo wa 1979, Sikinde ilipiga hodi tena na kumng’oa Juma Town, Abdallah Omary ‘Dulla’ na Mwanyiro na Juwata ikaenda Biashara Jazz kumchukua Hagai Kauzeni kuziba pengo la Mwanyiro katika gitaa zito.

Kutokana na Belesa kutokubalika kwa baadhi ya wanamuziki, aliamua kutimkia Bima Lee.

Chukuachukua hiyo ya wanamuziki ikafanya Msondo ipachikwe jina la Chuo cha Mafunzo na ikazidi kuonyesha kukomaa kwake ilipotunga kibao kilichokuwa na maneno ya “hii ni meli ya kuipakua tu”. Hata hivyo kibao hicho kilipigwa marufuku nchini na kilisikika zaidi Kenya.

Mwishoni mwa mwaka 1979, Juwata, ikitumia mtindo wa Msondo Ngoma, ilimchukua Shaaban Dede kutoka Dodoma International. Dede alikuwa na uwezo wa kutunga na kuimba vizuri sauti ya kwanza na kufukia mashimo yote yaliyoachwa na Bitchuka.

Mwaka 1982, DDC Mlimani Park ilipiga tena hodi na kumchukua Dede.

Iliimarisha muziki wake kwa kuongeza kinanda cha upepo (organ) kilichokuwa kikipigwa na Waziri Ally, aliyetokea Tanga na bendi ya The Revolution ambayo badaye ilijiita Kilimanjaro Band ‘Wana Njenje’. Baadaye Waziri alijikita zaidi na bendi hiyo ya muziki wa hotelini, badala yake Msondo ikamchukua Abdul Ridhiwani maarufu kwa jina la Pangamawe ‘Toto’.

Baada ya kutoa albamu kama Rabana, Piga Ua Talaka Utatoa, Ya Kale ni Dhahabu na Ajali, zilizotikisa nchi, Msondo ilianza kupoteza waimbaji wake. TX Moshi William, Joseph Maina, Suleiman Mbwembwe, Athuman Momba, Dede na Gurumo wote waliaga dunia na hivyo kuanza kutegemee kizazi kipya cha waimbaji kama Eddo Sanga, Juma Katundu na Hassan Moshi wanaouendeleza msondo.