Calisah: Niliuza gari kwenda kushiriki Mr Afrika

Mwanamitindo Calisah Abdulhamidu ‘Calisah’, amesema ilimlazimu kuuza gari ili kupata fedha kwa ajili ya kwenda kushiriki shindano la kumsaka Mr Afrika lililofanyika, Desemba 2, mwaka huu mjini Lagos nchini Nigeria, ambapo aliibuka mshindi.

Akizungumza na Mwananchi, Calisah alisema jambo hilo lilimsononesha ukizingatia kwamba alipita katika mamlaka zote zikiwamo zinazohusika na masuala ya sanaa miezi mitatu kabla kuomba kuwezeshwa, lakini hakuungwa mkono.

Pamoja na uamuzi huo wa kuuza gari, alisema fedha haikutosha na kulazimika kutafuta njia nyingine kupata ya kujazia.

Kama haitoshi, alisema wakati kila nchi ikiwa imepeleka washiriki zaidi ya watatu na kuwa na wasindikizaji kutoka serikalini, yeye alikuwa peke yake kama mtoto mkiwa.

Alisema mwaka huu aliamua kujitosa baada ya kulikosa shindano hilo zaidi ya mara mbili kutokana na kutokuwa na fedha licha ya kuletewa mwaliko na waandaji na anafurahi kuwa matunda yake ya kujitosa yameonekana.

Kutokana na hilo, aliishauri serikali na wadau wengine kubadilika ili kuiunga mkono uanamitindo badala ya kuwekeza katika mpira pekee.

“Nashukuru nimepata mikataba zaidi ya 12 mpaka sasa baada ya ushindi huo. Nitakuwa balozi wa taji hilo kwa mwaka mzima,” alisema Calisah.

Moja ya majukumu yake alisema ni kutembelea nchi mbalimbali za Afrika, kuzungumza na vijana ambao wanapitia matatizo mbalimbali ikiwamo utumiaji wa dawa za kulevya.

Katika shindano hilo jumla ya nchi 22, zilirusha karata zake na hatimaye Calisah kuibuka mshindi.