Facebook waondoa ukurasa unaomtetea R Kelly kuhusu kashfa inayomkabili

Muktasari:

  • Mtandao wa kijamii wa Facebook umeufunga ukurasa wa kumtetea mwanamuziki R Kelly uliokuwa umefunguliwa katika mtandao huo kwa madai ya kukiuka sheria za huduma

Mtandao wa kijamii wa Facebook umeufunga ukurasa ulioanzishwa kwa ajili ya kuwashambulia wanawake wanaomtuhumu nyota wa muziki wa Marekani, R. Kelly kwa maelezo kuwa unakiuka sheria za huduma.

Facebook iliufuta ukurasa huo Jumatatu baada ya wamiliki wa ukurasa huo unaoitwa Surviving Lies, kuposti maneno ya kushambulia angalau watu wawili kati ya wanaomtuhumu nyota huyo wa miondoko ya R&B aliyetamba na wimbo wa “I Believe Can Fly”.

R. Kelly, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 51, anaandamwa na kashfa ya kuwanyanyasa kingono wasichana wenye umri mdogo, lakini amekuwa akikanusha vikali kuhusika.

Tangu Januari 7, 2019 baada ya kusambaa kwa video ya Surviving R Kelly yenye wanawake wanaomtuhumu nyota huyo kuwa aliwanyanyasa kingono walipokuwa na umri mdogo.

Inadaiwa kuwa video hiyo ilimfanya R Kelly na kambi yake kujibu mapigo kwa kufungua ukurasa wao walioupa jina Surviving Lies.

Ukurasa huo unatumia picha ya katuni maarufu ya Pinocchio, ambaye pua yake huongezeka urefu kadri anavyodanganya.

Tovuti ya TMZ imeeleza kuwa lengo la ukurasa huo ni kumsafisha Kelly na kuwapuuza waliokuwa wakilalamika dhidi yake.

Moja ya posti kwenye ukurasa huo ilikuwa inahoji: “Kwa nini ushahidi huu unapuuzwa. Wewe uwe hakimu.”

Katika video ya makala yenye sehemu sita, ambayo ilirushwa kuanzia Alhamisi hadi Jumamosi, kuna ushuhuda wa wanawake hao wanaomtuhumu Kelly, pamoja na mahojiano na washirika na ndugu wa R.Kelly.

Wanawake hao wanakanusha kuhusu yaliyozungumzwa kwenye video ya awali iliyomuhusisha pioa mke wa zamani wa gwiji huyo wa R&B, Andrea Kelly.
Hadi Jumatatu, tayari ukurasa huo ulikuwa na wafuasi 5,000 waliokuwa wakijadili mada za kumtetea mwanamuziki huyo, wakiwa pia wametuma picha za posti zinazodaiwa za mawasiliano kati ya wanawake hao na R. Kelly.

Katika taarifa yake, Facebook imesema: "Hatukubali kuona watu wakitoa maelezo ya mtu binafsi yenye lengo la kumtetea kupingana na wengi na kupotosha uhalisia inakiuka sera na taratibu zetu.”

Mwakilishi wa R. Kelly alikataa kuzungumzia ukurasa wa Surviving Lies alipofuatwa na waandishi wa habari.