HEKAYA ZA MLEVI: Jiko la shamba linapendeza na kisamvu

Gaston Nunduma

Nilipokuwa mdogo nilikuwa mkorofi sana. Niliweza kuanzisha ugomvi katikati ya watoto tuliocheza nao mechi hadi wakatawanyika. Wengi walijiuliza nilitegemea nini wakizingatia kuwa nilikuwa na umbo dogo kuliko umri wangu.

Siku moja nilimsimamisha ‘mtemi’ wa Uswazi na kuamuru arudishe senti aliyoipora kwa mtoto wa kota. Jamaa alilitazama jumbo lake, akanishangaa. Na mimi bila kupepesa macho nilinyosha mkono kuamuru anipatie. Akakunja ndita na kunipatia huku akijiuliza. Mimi nikamkabidhi mwenye mali yake na kumkosa kibao; “kimbia!” Yule mtoto alikimbia bila kuangalia nyuma, nami nikaondoka kibabe nikimwacha mtemi yule akiduwaa.

Sikuwa na ubavu wa kupigana ila nilitegemea mbio. Ilikuwa ukinikosa ngumi tu, hutaliona hata vumbi langu. Na Mungu bariki nilikuwa na mbio kama paa. Wakati mwingine niliona raha kufukuzwa na kundi la watoto ishirini niliowaacha hatua nyingi nyuma yangu. Nilijiona kama bingwa wa mbio ndefu nikishangiliwa na maelfu ya Watanzania pale Uwanja wa Taifa.

Lakini siku moja niliyakanyaga kwa bonge mmoja aliyeitwa Kulakula. Alikuwa na mabavu na asiye na huruma hata kidogo. Huyu jamaa alikuwa na kawaida ya kuomba chochote kilichoweza kuliwa. Akikuona na embe basi kabla hujalimenya utakuta tayari yupo mbavuni kwako. Si kwamba alikuwa na njaa, hapana. Bali amuonapo mwenzie akila hudhani kuwa anafaidi kuliko yeye anapokula.

Siku moja mimi nilikuwa na karanga nyingi nilizochemshiwa na mama yangu nyumbani. Wakati wa mapumziko nilitoa mfuko na kuwagawia wote niliokuwa nao. Nikabakiza kidogo ambazo ningezila baadaye wakati wa kipindi cha michezo. Kulakula hakukubali. Akanivizia nilipokuwa mpirani na kuniibia zote. Nilichukia na kusema ni lazima nitamwonyesha.

Mwalimu wetu mkuu aliishi katika eneo la shule. Alikuwa mfugaji mzuri wa kuku, bata na mbuzi. Nikaokota punje za mavi ya mbuzi. Kisha nikanunua karanga za kukaangwa zilizopimwa kwa kikombe, nikazitia kwenye mfuko wa karatasi. Nikachukua mfuko kama huo, nikachanganya na karanga kidogo na ile mbolea kidogo. Kama kawaida nilizigawa karanga kwa wadau na mara Kulakula akanipiga “full light”, akaja mbio mkono mmoja ukiwa mbele.

Haraka niliubadili mfuko na kuutanguliza ule wenye ‘miksa’ ya karanga na mbolea. Pasi na simile Kulakula akaingiza mkono kwenye mfuko, akachota na kubwia. Kwa spidi ya umeme mkono ukaanza kutuzungukia ili tumchangie tulizokuwa tukila. Hata hivyo ladha ya karanga za leo ilimtatiza Kulakula: “Ni sawa kuna ka-chumvi kama kawaida, lakini mbona wote wananitazama miye?”

Kwa bahati mbaya sana mmoja wetu alishindwa kujizuia, akacheka kwa nguvu. Awali ya yote Kulakula alinidaka ukosi wa shati. Na mimi kwa spidi zaidi ya umeme nikalivua na kumwachia. Nikala kona moja kwa moja nyumbani.

Kwa bahati baba na mama walikuwa waajiriwa serikalini, hivyo nilimwongopea dada wa kazi kuwa nilianguka kwenye tope na nimeliacha shati linafuliwa shuleni.

Sikuwa na nia mbaya kumuadhibu Kulakula. Pengine nilichokosea ni aina ya adhabu niliyotoa. Wakati wa utoto hatukuwa na uwezo wa kutafakari madhara ya siku zijazo. Tuliwaza ya siku hiyo tu na ndiyo maana tulipewa mafunzo yaliyoonyesha siku hiyo tu. Ulishawahi kusikia kuwa ukitenda mema unakwenda peponi ambako utakuta ubwabwa, zabibu, doriyani, forosadi na vikorokoro vyote vya kuchezea. Ungeambiwa kuwa peponi kuna shule usingetenda mema kwa sababu ungemfananisha mwalimu wa hesabu wa huko na huyu uliye naye shuleni kwako.

Nilitaka kumfundisha Kulakula kuwa kila kinachozidi mwilini huwa kina madhara. Binadamu hana budi kula protini, lakini protini hiyohiyo ikizidi ni lazima atakuwa na hali mbaya kiafya.

Kulakula anapaswa kutambua kuwa simba hali majani kwa sababu ya kuwa na njaa, bali anatafuta virutubisho visivyokuwemo kwenye nyama. Vilevile nyati hajawa “mwili nyumba” kwa kula mafuta. Yeye hula majani tu siku zote.

Nina maana kuwa sio ujanja kula kila kinachokutamanisha. Pita kando ya mkaanga chipsi hapo barabarani. Agiza chipsi yai, “zege” na firigisi za kuku. Mwache akamulie tomato sosi na chili (usitokwe na udenda, kazi inaendelea). Baada yote usile chakula hicho, bali kipeleke kwa mkemia akakupimie vilivyomo humo. Atakapokupa jibu hakika utamrudia muuza chipsi kugombana naye.

Chochote kinachozidi mwilini huwa sumu. Chumvi ikikosekana kwenye chakula huwa tatizo, lakini ikizidi huweza kuwa tatizo kubwa zaidi. Elimu ya utoto ilikataza kula ovyo kama zinavyokataza elimu ya wakubwa.

Wengine tulitishwa kuwa tumbo litajaa na chakula kitakwenda mgongoni. Tulikuwa tukimwona mtu aliyepinda mgongo tulidhani kuwa tumbo lake lilijaa.

Kwetu mama mjamzito alikatazwa kula mayai asije kuzaa mtoto kipara. Lakini ukweli ulikuwa ni kumuepusha na upasuaji wakati wa uzazi. Mama anapokula mayai mtoto naye huvimbiana tumboni. Hivyo kulifanya suala la uzazi kwa njia ya kawaida kushindikana.

Vitabu vya dini na imani vinakazia suala la kufanya mambo kwa kiasi. Kula sana ama kula hovyo ni kosa kubwa. Japokuwa havikutaja kiasi unachotakiwa kula.

Lakini kwa vile ulipewa akili ni lazima ujue kuwa tembo anaruhusiwa kula kiasi gani ili aende sawa na mwili wake. Vilevile ukapewa na hekima ya kutojaribu kumgeza tembo jinsi anavyojisaidia. Ni hatari kubwa.