Jinsi ya kupika samaki wa mvuke

Muktasari:

  • Chukua bakuli ndogo na weka kitunguu saumu, sosi ya samaki, chumvi, ndimu maji, sukari na pilipili iliyokatwa katwa , kisha katikatia majani ya kijani ya vitunguu na weka pembeni.

Ili kupunguza kiasi cha karoli katika chakula, namna sahihi ya kumpika ni kutumia mvuke. Samaki aliyepikwa  kwa namna hii mbali ya kuwa mtamu, pia ni mzuri kwa afya kuwa virutubishi vyake hubaki kama vilivyo tofauti na wale wa kukaanga au kupikwa kwa namna nyingine.

Mahitaji

Samaki mzima anaweza kuwa  changu au aina nyingine

Kitunguu saumu kilichopondwa vijiko vitatu

Pilipili zilizoiva kiasi

Juisi ya ndimu au limao robo kikombe cha chai

Sosi ya samaki

Sukari kijiko kimoja  cha chai

Maji vijiko vitatu vya chai

Majani ya vitunguu maji

Majani matatu ya mchaichai

Majani ya kotmiri/  Celery

Jinsi ya kupika

Chukua bakuli ndogo na weka kitunguu saumu, sosi ya samaki, chumvi, ndimu maji, sukari na pilipili iliyokatwa katwa , kisha katikatia majani ya kijani ya vitunguu na weka pembeni.

Baada ya hapo chukua samaki wako na muoshe vizuri na mtoe magamba kama anayo. Hakikisha unamkata mkia ili aenee kwenye chombo unachomuweka kwa ajili ya kumpika kwa mvuke. Chombo hicho kinaweza kuwa sahani iliyotumbukia kwani atakapoiva atatoa supu kidogo. Chukua chumvi , changanya na juisi ya ndimu kisha mpake samaki wote . Hakikisha eneo la katikati unalipasua kidogo ili kurahisisha mchanganyiko wako kupenya kwa urahisi ndani yake. Kabla ya kuweka samaki kwenye chombo hakikisha unaweka majani ya mchaichai chini yake.

Chukua sufuria kubwa na weka maji kisha weka bakuli ya bati ndani yake. Kisha juu ya bakuli weka sahani yako ya samaki na kisha funika. Acha maji hayo yachemke kwa dakika saba hadi kumi.

Baada ya hapo samaki wako atakuwa ameiva vizuri. Toa sahani yako ya samaki na kisha iweke juu ya meza kawa ajili ya kuweka  viungo. Chukua majani ya giligilani au celery na kisha katia katika kuzunguka samaki. Baadaye miminia ule mchanganyiko uliotengeneza kwenye bakuli. Samaki wako yuko tayari kwa kuliwa.