MH. JOKATE MWEGELO: Nini Samatta,kwake kuna Msuva,Kaseja

NADHANI unafahamu, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo ni Yanga wa kulialia, lakini linapokuja suala la uongozi bora huwa hapepesi macho unaambiwa.

Licha ya kuipenda Yanga kutoka ndani ya sakafu wa moyo wake, amefunguka mazima anatamani kuliona chama lake hilo likifuata njia inazopitia Simba kwa sasa.

Amesema anatamani Yanga ambayo kwa sasa haiko vizuri kutokana na mgogoro wa uchaguzi na mdodoro wa kiuchumi na anafahamu, Simba ina viongozi wenye maono na mawazo ya kijanja katika kujenga taasisi imara.

“Uongozi wa Simba unaonyesha dhamira ya kufanya kitu kikubwa na tofauti katika soka la Tanzania, mimi ni shabiki wa Yanga, lakini natamani timu ninayoipenda ijifunze kitu tofauti kutoka Simba.

“Kama unaiangalia Simba utabaini ina watu makini kuanzia kwa msemaji wake, Haji Manara na safu nzima ya vigogo wa juu, ambao wanaifanya timu kuwa bora ndani na nje ya uwanja.

“Hapa nazungumzia uongozi na mfumo wake tu, ila kuhusu matokeo ni suala la kiufundi, hapa Yanga haiwezi kukimbia ni lazima ijifunze ili siku moja nijivunie uongozi bora wa timu ninayoipenda,” anasema DC huyo wa kishua anayeing’arisha Kisarawe na kuiweka kwenye anga nyingine kabisa.

Mwandishi wa makala haya alitia timu ofisini kwa mkuu huyo wilaya, ambaye pamoja na mambo mengi alieleza jinsi anavyovutiwa na mastaa wawili wa Tanzania.

Lakini kama unadhani kwenye orodha ya DC Jokate kuna jina la straika maarufu wa Kitanzania anayekipiga Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, basi utakuwa umechana mkeka wako. Hebu msikie mwenyewe hapa.

Swali: Umesema wewe ni shabiki wa Yanga, mchezaji gani anayekupa mzuka zaidi uwanjani?

Mwegelo: Ukweli kutoka moyoni namkubali sana straika anayekipiga Klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco, Simon Msuva.

“Msuva alionekana mchezaji wa kawaida tu, lakini amepambana na kutengeneza jina na leo brand yake ni kubwa na kuna watu wengi wanavaa jezi zenye jina lake.

“Napenda staili ya soka lake uwanjani, nadhani ndiyo imemsaidia kuwa mchezaji wa kimataifa na kutoka kimaisha. Kama una bidii, basi soka sio kazi ngumu, lakini inahitaji uwekezaji wa mhusika kisha watu wengine watakuja kuwekeza kwako.

“Amefanikiwa na sasa Jadida imewekeza kwake kwa sababu inanufaika na huduma anayoipa. Pia, kuna mchezaji mwingine ambaye ninamzimia sana huyu ni kipa, Juma Kaseja, ambaye kwa sasa anakipiga pale KMC.

“Kaseja ametengeneza brand yake na kuwa maarufu sana, hawezi kukatiza mahali kisha watu wasifahamu kama amepita. Brand inasaidia watu kufilka mbali kwa sababu kuna maisha nje ya soka, lakini inategemeza zaidi ulifanya nini ulipokuwa na nafasi

“Nadhani unaona kwa wachezaji wakubwa Ulaya waliofanya vizuri baada ya kustaafu wanakwenda kuchambua na kutangaza soka kwenye vituo vikubwa vya runinga, bila kuwa umefanya kitu huwezi kupata nafasi kama hiyo.”

Swali: Ushindani wa soka hapa nchini ukoje?

Mwegelo: Tunarudi kulekule, kama wachezaji hawajaamua kuwa wachmastaa bado hatutaona ushindani wa kweli uwanjani. Ila ninachokiona Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kuwekeza kwenye michezo ikiwamo soka.

“Wapenda michezo kama mimi walifarijika sana na hatua ya Rais John Magufuli kutoa fedha kusaidia maandalizi ya Timu ya Taifa, Taifa Stars na alitazama mechi japo hatukupata matokeo mazuri, lakini tutafika tu.”

Swali: Rais Magufuli kutoa fedha na kutizama timu ya taifa ikicheza, ina maana gani kwa wachezaji?

Mwegelo: Inamaanisha wana deni kubwa la kulipa kwa mashabiki wa soka, lakini kwa uongozi wa juu kabisa wa nchi uliowaamini.

Hivyo, watalipaje fadhila hizo ni kwa kuwapa raha mashabiki kwa kupata matokeo mazuri.

Kimsingi mashabiki wa soka wana kiu ya ushindi...timu zitupe raha tujivunie kupenda michezo.

Swali: Asante sana mheshimiwa

Mwegelo: Karibu sana.