Mhina wa bendi ya Tanzanite afariki dunia

Muktasari:

Mwanamuziki huyo na bendi yake wamewahi kutumbuiza jukwaa moja na Michale Jackson

Dar es Salaam. Mwanamuziki wa bendi ya Tanzanite, John Mhina amefariki dunia leo Alhamisi Julai 12, 2018 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Akizungumza na MCL Digital, mdogo wa marehemu, Joseph Mhina amesema John amefariki dunia leo alfajiri nyubani kwake Bunju.

Amesema kwa muda wa wiki tatu mpaka mauti inamkuta, John hakuwa katika hali nzuri kiafya na kwamba alikuwa akitumia dawa za ugonjwa wa moyo uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.

John ambaye akiwa na bendi hiyo walitoa nyimbo nyingi zilizopendwa miaka ya 80 ikiwemo Pugu Kariakoo na Nimekota Kidude, pia amewahi kuimba jukwaa moja na marehemu Michael Jackson.

Akizungumza na MCL Digital leo, Katibu wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata),  Hassan Msumari  amesema Mhina na bendi yao waliochangia kuleta mapinduzi katika muziki wa dansi kwa kupiga muziki kisomi na kisasa zaidi.

“Walipata mialiko mbalimbali nchini Japan, Marekani, Dubai na kwingineko. Pia walipata bahati ya kutumbuiza na Michael Jackson, mwanamuziki ambaye kila mtu alitamani kufanya nae kazi,” amesema.

Amesema bendi hiyo nchini ilikuwa ikitoa burudani ya muziki katika hoteli kubwa, kujizolea mashabiki lukuki.

Wanamuziki King Kiki na Ally Zahir Zorro wamemzungumzia marehemu, kubainisha kuwa alikuwa mtu aliyeheshimu kazi yake.